1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi latangaza kukombolewa sehemu ya Jebel Marra

Admin.WagnerD9 Februari 2016

Jeshi la Sudan limewataka raia warejee kwenye makaazi yao, baada ya kuyakimbia kutokana na mapigano ya wiki mbili katika eneo la milima la Jebel Marra kwenye jimbo la Darfur.

https://p.dw.com/p/1Hru9
Sudan Omar al-Bashir Präsident
Rais wa Sudan Omar al- BashirPicha: Getty Images/AFP/E. Hamid

Maalfu ya raia wa sehemu ya milima ya Jebel Marra waliyakimbia makaazi yao kutokana na mapigano baina ya majeshi ya serikali na waasi katika jimbo hilo la Darfur magharibi mwa Sudan.

Kwa mujibu msemaji wa Umoja wa Mataifa maalfu ya watu walikimbilia upande wa kaskazini wa eneo la Jebel Marra katika jimbo hilo. Eneo la milima la Jebel Marra ndiyo ngome kuu ya jeshi la waasi linaloongozwa na Abdulwahid Nur. Majeshi ya serikali yamesena sasa yanaidhibiti tena sehemu hiyo na yamewataka raia warejee.

Msemaji ,wa jeshi hilo Brigadia Ahmed Khalifa al - Shami ametangaza kwamba wananchi wanaweza kurejea kwenye vijiji vyao. Brigadia al- Shami amehakikisha kwamba jeshi la serikali limeimarisha udhibiti wa barabara na sehemu zote muhimu.Amesema majeshi ya serikali yanaendelea na juhudi za kuzikomboa sehemu chache zilizobakia katika eneo hilo la Jebel Marra.

Waasi wakanusha madai ya serikali

Kiongozi wa jeshi la waasi Abdulwahid Nur amekayanusha madai ya jeshi la serikali. Amekanusha taarifa kwamba wapiganaji wake wamelipoteza eneo la Jebel Marra katika jimbo la Darfur. Abdulwahid Nur ameliambia shirika la habari la AFP , kutokea nchini Ufaransa kwamba tangu mwezi uliopita majeshi ya serikali yamekuwa yanawashambulia wapiganaji wake kutokea sehemu mbalimbali.

Ameyaelezea mapigano hayo kuwa ni maafa kutokana na jumuiya ya kimataifa kunyamaza kimya.

Mwito wa jeshi la serikali kuwataka raia warejee kwenye makaazi yao umetolewa baada ya Umoja wa Mataifa kutahadharisha juu ya hali mbaya iliyokuwa inawasibu maalfu ya raia waliogeuka wakimbizi wa ndani. Mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Marta Ruedas amesema watu hao wanahitaji kila aina ya msaada.

Umoja wa Mataifa watoa misaada katika jimbo la Darfur
Umoja wa Mataifa watoa misaada katika jimbo la DarfurPicha: picture-alliance/dpa/A. Gonzales

Mwandishi:Mtullya Abdu.afpa,dpae,

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman