1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Radovan Karadzic kusomewa mashtaka leo alaasiri

Nijimbere, Gregoire31 Julai 2008

Kiongozi wa zamani wa Wasabu wa Bosnia Radovan Karadzic atafikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa ya jinai ya mjini The Hague Uholanzi hii leo kwa mara ya kwanza kusomewa mashtaka 11 yanaoyomkabili.

https://p.dw.com/p/Ennc
Radovan Karadzic, kiongozi wa zamani wa Wasabu wa BosniaPicha: picture-alliance/ dpa

Radovan Karadzic atakuwa mbele ya jaji Alphons Orie wa mahakama ya kimataifa ya jinai kwa ajili ya Yugoslavia ya zamani leo alaasiri saa 10 majira ya hapa Ujerumani na Afrika ya kati.

Jaji huyo atamsomea Radovan Karadzic mashtaka yote 11 yanayomkabili.

Geert-Jan Gericht, wakili wa zamani kwenye mahakama za Umoja wa mataifa, akizungumza juu ya utaratibu wa kisheria, anasema lazima Radovan Karadzic ajibu:

“Kuna mashtaka 11 atakayosomewa.

Lazima na yeye mara 11 akubali ama akane mashtaka hayo 11”.

Kulingana na mwendeshamashtaka wa mahakama hiyo ya kimataifa ya jinai kwa ajili ya Yugoslavia ya zamani ambayo ni sehemu ya mahakama ya kimataifa ya jinai ya mjini The Hague Uholanzi, Serge Brammertz , mashtaka hayo 11 ni pamoja na mauaji ya kuangamiza jamii, uhalifu wa kivita na ukiukaji wa haki za binaadamu. Hasa, Radovan Karadzic anatuhumiwa kuwahamisha watu kwa nguvu kwa misingi ya kikabila, kuwakandamiza wakaazi wa mji wa Sarajevo, kuamrisha mauaji ya kuangamiza jamii katika kijiji cha Sebrenica mnamo mwezi Julai mwaka 1995 ambapo waislamu kiasi ya 8.000 wanamume na wavulana waliuawa.

Mbali na hayo, Radovan Karadzic anatuhumiwa kuhusika na kuwashikilia mateka wafanyakazi na wanajeshi wa Umoja wa mataifa wa kulinda amani.

Lakini daima kulingana na mwendeshamashtaka Serge Brammertz, maandalizi ya kesi yenyewe, yatachukuwa muda mrefu: “Itachukuwa miezi kadhaa kabla ya upande wa mashtaka na upande wa utetezi kuwa tayari kuanza kesi. Kama nilivyosema hapo kabla, huwa tunaanza kuyapitia tena mashtaka yote ili kufikisha mahakamani faili iliyokamilika. Lakini siwezi sasa hivi kukisia muda wa matayarisho hayo na niseme ni miezi ngapi”.


Baada ya kesi kuanza, huenda mambo yakaenda haraka, kwani mwendeshamashtaka Serge Brammertz ameongeza kusema kuwa, lengo lao muhimu ni kuepuka kesi ndefu.

Radovan Karadzic alisema atajitetea mwenyewe kama rais wa zamani wa Yugoslavia ya zamani Slobodan Milosevic ambae alifariki dunia kwa maradhi ya moyo mwaka 1996 akiwa ndani ya gereza la mahakama ya kimataifa ya jinai hapo mjini The Hague Uholanzi.


Ikiwa Radovan Karadzic atapatikana na hatia, anakabiliwa na athari ya kukatiwa kifungo cha maisha jela. Radovan Karadzic, mwenye umri wa miaka 63 sasa, alikamatwa wiki iliyopita mjini Belgrade mji mkuu wa Sabia, baada ya kusakwa kwa kipindi cha miaka 13.