1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Radovan Karadzic apelekwa kwenye mahakama ya kimataifa ya jinai The Hagu...

Nijimbere, Gregoire30 Julai 2008

Kiongozi wa zamani wa Wasebu wa Bosnia Radovan Karadzic anayetuhumiwa kuhusika na makosa ya jinai katika vita vya Bosnia-Herzegovina, amepelekwa katika mahakama ya kimataifa ya jinai The Hague Uholanzi.

https://p.dw.com/p/EmY8
Radovan Karadzic akiwa bado kiongoziPicha: picture-alliance/ dpa

Ndege ambayo imemsafirisha Radovan Karadzic imetua kwenye uwanja wa ndege wa mjini Rotterdam kusini magharibi mwa Uholanzi kabla ya kusafirishwa kwa gari hadi mjini The Hague makao ya mahakama ya kimataifa ya jinai. Radovan Karadzic anakabiliwa na tuhuma za mauaji ya kuangamiza jamii, uhalifu wa kivita na makosa mengine dhidi ya binaadamau wakati majeshi yake yalipoukalia mji wa Sarajevo na hasa mauaji ya waislamu kiasi ya alfu 8 katika kijiji cha Sebrenica ambayo ndiyo mauaji makubwa barani Ulaya tangu kumalizika vita vikuu vya pili vya dunia.

Radovan Karadzic amepelekwa uwanja wa ndege kutoka jela la mjini Belgrade na polisi maalum wa idara ya upelelezi waliojifunika nyuso na wakiwa katika gari zenye rangi nyeusi.


Katika jela ya mahakama ya kimataifa ya jinai ya mjini The Hague, Radovan Karadzic atawakuta watuhumiwa wengine 37 waliokamatwa kuhusiana na uhalifu wa kivita wakati wa kivita hivyo vya Bosnia-Herzegovina.

Kila mfungwa anachumba chake kikubwa ambacho kina kitanda, jiko na huduma nyingine muhimu. Kuna pia Televisheni na viwanja vya michezo mbali mbali ndani ya gereza ambako pia wafungwa wataweza kuvuta hewa kila siku. 

Mbali na wafungwa hao kuhusiana na vita vya Yugoslavia, Radovan Karadzic atawakuta pia wafungwa wengine 5 wanazuwiliwa kwa uhalifu wa kivita akiwemo rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor. Kulingana na waandamizi wa jela ya Scheveningen ya mahakama hiyo ya kimataifa ya jinai ya mjini The Hague, mfungwa hupewa chumba bila kujali kabila, dini au asili yake.


Jana mji mkuu wa Sabia Belgrade ulishuhudia maandamano makubwa ya watu kiasi ya alfu 10 wanaopinga kumpeleka Radovan Karadzic kwenye mahakama ya kimataifa ya jinai ya mjini The Hague Uholanzi wakimtaja Karadzic shuja ambae aliyanusuru maisha ya wasabu wengi katika vita vya Bosnia-Herzegovina mwanzoni mwa miaka ya 90.

Watu 45 wengi wao wakiwa ni polisi wa usalama walijeruhiwa katika mapambano kati ya waandamanaji na polisi.

Kulingana na wadadisi wa maswala ya kisiasa kumpeleka Radovan Karadzic kulikuwa muhimu kwa serikali mpya ya Sabia inayotaka kuwa na uhusiano mzuri na Umoja wa Ulaya wakiksudia nchi yao hata kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Pia serikali katika kumhamisha Radovan Karadzic mjini The Hague, inatarajia kupunguza hali ya kutisha iliyozushwa na kukamatwa kwa kiongozi huyo wa zamani wa kisabu siku chache zilizopita na kuepusha maandamano zaidi.

Radovan Karadzic alikamatwa wiki moja iliyopita katika mji mkuu wa Sabia Belgrade baada ya msako wa miaka 11. Mshirika wake wa karibu katika vita hivyo vya Bosnia-Herzegovina, jenerali Radko Mladic bado hajakamatwa.