1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Qatar yawatimua wanadiplomasia wa Chad

Sylvia Mwehozi
25 Agosti 2017

Qatar imeamuru kufungwa kwa ubalozi wa Chad na kuwapatia masaa 72 wanadiplomasia wake kuondoka, huku ikirejesha mahusiano kamili ya kidiplomasia na taifa lenye nguvu kikanda la Iran. 

https://p.dw.com/p/2ipSM
Katar Doha italienischer Außenminister Angelino Alfano und Sheikh Mohammed bin Abdulrahman al-Thani
Picha: picture-alliance/AA/M. Farag

Ingawa Qatar imekuwa katika msuguano na mataifa manne ya Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu kwa madai kwamba nchi hiyo inafadhili ugaidi, siku ya Jumatano, Chad ilijiunga na mataifa machache ya Kiafrika ambayo yalijitosa kwenye mzozo huo kwa kusema kuwapa wanadiplomasia wa Qatar siku 10 tu kuondoka, nayo ikiituhumu Qatar kwa kujaribu kudhoofisha taifa hilo la Afrika ya Kati kupitia jirani yake wa kaskazini, Libya.

Wizara ya mambo ya nje ya Qatar imesema jana Alhamis kwamba uamuzi wa Chad unaonyesha dhahiri kwamba ina nia ya kujiunga na kampeni ya usaliti wa kisiasa dhidi ya taifa hilo kama mataifa mengine yaliyoitenga kwa sababu zile zile. Senegal ilisema wiki hii kwamba imemrejesha balozi wake kwa Qatar baada ya kumuondoa miezi mitatu iliyopita katika jaribio la kuhimiza suluhisho la amani kwa mgogoro huo. Chad, hata hivyo, haikutoa maelezo ya kina kuunga mkono madai yake kwamba Doha inajaribu kuidhoofisha kupitia Libya.

Katar Iranische Botschaft in Doha
Ubalozi wa Iran mjini Doha Picha: Imago/Karo

Umoja wa Falme za Kiarabu na Qatar ambazo kwa pamoja zilikuwa na jukumu muhimu katika kuwaunga mkono waasi waliomuondoa Muammar Gaddafi mwaka 2011 nchini Libya, sasa zimekuwa ni mahasimu katika uwanja wa mapambano kwa maslahi tofauti katika taifa hilo la kaskazini mwa Afrika.

Huku hayo yakiendelea, Qatar imerejesha mahusiano kamili ya kidiplomasia na taifa lenye nguvu kwenye Ghuba, Iran, ikiwa ni hatua muhimu katikati mwa msuguano wa kidiplomasia na majirani zake wa Kiarabu. Taarifa kutoka wizara ya mambo ya nje inasema Qatar ina lengo la kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizo mbili ambazo zina hazina kubwa ya gesi asilia duniani.

Sehemu ya taarifa hiyo imesomeka hivi: "Taifa la Qatar linatangaza leo kwamba balozi wake kwa Tehran atarudi kuendelea na majukumu yake ya kidiplomasia". Qatar pia ilikuwa inajaribu "kuimarisha mahusiano ya pande mbili na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyanja zote", imeongeza taarifa hiyo.

Symbolbild Katar und Iran
Bendera za Qatar na Iran Picha: Colourbox/A. Mijatovic

Mjini Tehran kwenyewe, wizara ya mambo ya nje ilisema uamuzi wa Qatar ulifuatiwa na mazungumzo kwa njia ya simu Jumatano usiku kati ya Waziri wa Mambo ya Nje Mohammad Javad Zarif na mwenzake Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani. Doha ilimuondoa balozi wake kutoka Tehran mwezi Januari 2016 kufuatia mashambulizi kwenye ubalozi wa Saudi Arabia, yaliyochochewa na uamuzi wa Riyadh wa kutekeleza hukumu ya kifo kwa kiongozi wa kidini wa Kishia katika nchi hiyo.

Uamuzi wa kurejesha mahusiano kamili ya kidiplomasia unakuja wakati Qatar ikiwa imefungwa katika mgogoro wa kidiplomasia na mpinzani mkubwa wa Iran kikanda, Saudi Arabia ambaye anayeituhumu Doha kuwa na mahusiano na Washia wa Iran na kuunga mkono makundi ya Kiislam ya Kisunni yenye itikadi kali.

Juni 5 mwaka huu, mataifa ya Saudia Arabia, Misri, Bahrain na Falme za Kiarabu yalivunja uhusiano wa kidiploamasia na biashara kwa Qatar katika moja ya mgogoro uliokuwa mbaya kulikumba eneo la ukanda wa Ghuba katika karne. Kwa ajabu mgogoro huo inawezekana kuwa umeyasukuma mataifa ya Iran na Qatar kuwa karibu zaidi.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reters/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef