1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

PYONGYANG: Korea Kaskazini yaonywa isifanye jaribio la kinyuklia

4 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD6M

Mataifa yenye uwezo mkubwa duniani yameionya Korea Kaskizini isifanye jaribio la kinyuklia, ikijibu uhasama wa Marekani dhidi ya utawala wake. Marekani, Umoja wa Ulaya, Urusi na Japan, zimeionya serikali mjini Pyongyang, ijizuie kwani jaribio lolote la kinyuklia litazorotesha usalama katika eneo hilo na ulimwenguni kote kwa jumla.

Marekani imesema jaribio la kinyuklia litaifanya Korea Kaskazini itwengwe zaidi.

Korea Kaskazini imetishia itafanya jaribio la kinyuklia, lakini haikutaja tarehe. Mara kwa mara Korea Kaskazini imekuwa ikisema ina silaha za kinyuklia lakini haijawahi kufanya majaribio yoyote kuthibitisha madai hayo.

Wakati huo huo, Korea Kusini imeitolea mwito Korea Kaskazini ifutile mbali mpango wake wa kufanya jaribio la kinyuklia na irudi katika mazungumzo ya kimataifa kuhusu mpango wake wa nyuklia.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Korea Kusini, Choo Kyu-ho amesema mjini Seoul kwamba nchi yake haitaivumilia Korea Kaskazini inayomilliki silaha za kinyuklia.