1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

PYONGYANG: El Baradei azuru Korea Kaskazini

13 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCJW

Kiongozi wa shirika la kimataifa la kuzuia usambazaji wa silaha za kinyuklia, IAEA, Mohamed El Baradei, amewasili mjini Pyongyang kwa mazungumzo na viongozi wa Korea Kaskazini.

Lengo la ziara yake ni kuishawishi nchi hiyo iwaruhusu wachunguzi wa shirika hilo warejee tena nchini humo.

El Baradei anafanya ziara yake mwezi mmoja tangu makubaliano ya kihistoria yalipofikiwa wakati wa mazungumzo ya mataifa sita mjini Beijing China yaliyoongeza matumaini kwamba Korea Kaskazini hatimaye itaachana na mpango wake wa silaha za kinyuklia.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Korea Kaskzini iliahidi itawaruhusu wachunguzi wa Umoja wa Mataifa kufanya uchunguzi katika vinu vyake na kukifunga kinu chake cha nyuklia katika kipindi cha siku 60.

Kwa kufanya hivyo Korea Kaskazini ingepewa tani elfu 50 za mafuta na uwezekano wa kuongezewa tani milino moja zaidi katika siku za usoni.