1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin: Uturuki itajutia kitendo chake

3 Desemba 2015

Vita vya maneno kati ya Urusi na Uturuki vimeendelea, baada ya Rais Vladmir Putin wa Urusi kuapa kuwa Uturuki itajutia kitendo chake cha kuidungua ndege ya kivita ya Urusi katika eneo la mpaka nchini Syria.

https://p.dw.com/p/1HGuK
Rais wa Urusi, Vladmir Putin
Rais wa Urusi, Vladmir PutinPicha: Reuters/S. Karpukhin

Akiwahutubia wabunge katika hotuba yake ya mwaka kwa taifa, ambayo pia imezungumzia mashambulizi ya anga nchini Syria, Rais Putin, ameahidi kulipiza kisasi kutokana na kitendo hicho cha Uturuki na kwamba hawatasahau uhalifu uliofanywa na magaidi.

''Lakini kama kuna mtu yeyote anayehisi kafanya uhalifu huu mbaya wa kivita, kuwaua watu wetu, kwamba wataepuka kuchukuliwa hatua, wamekosea sana. Tutawakumbusha kwamba kile walichokifanya zaidi ya mara moja, na watajutia kile walichokifanya zaidi ya mara moja. Na tunajua hasa nini kinapaswa kufanyika,'' alisema Putin.

Wiazara ya Ulinzi ya Urusi imemshutumu Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan na familia yake kwa kufaidika katika biashara ya mafuta na kundi lenye itikadi kali la Dola la Kiislamu-IS, ambalo linadhibiti eneo kubwa la Syria, ikiwemo visima kadhaa vya mafuta.

Rais Putin amesema wanafahamu nani anawapatia fedha Uturuki na kuwaruhusu magaidi kujipatia fedha kutokana na mafuta yanayoibwa Syria. Amesema hatoipuuza hatua ya Uturuki kuwasaidia magaidi.

Erdogan akanusha madai dhidi yake

Amesema ni wazi kutokana na fedha hizo, magaidi wanawapa kazi mamluki, wanaonunua silaha na kupanga mashambulizi ya kigaidi dhidi ya raia wao, raia wa Ufaransa, Lebanon, Mali na nchi nyingine.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip ErdoganPicha: Getty Images/AFP/A. Altan

Hata hivyo, Rais Erdogan amekanusha madai hayo dhidi yake, akisema Uturuki ina ushahidi kwamba Urusi ndiyo inayohusika katika biashara ya mafuta na kundi la IS nchini Syria na kwamba wataziweka hadharani taarifa hizo.

Erdogan amerudia kusema kuwa atajiuzulu iwapo Urusi itatoa ushahidi kuhusu madai hayo. Amesema George Haswani, mwenye pasi ya kusafiria ya Urusi na raia wa Syria, ni mmoja kati ya wafanyabiashara wakubwa wanaoununua mafuta kutoka kwa IS. Amesema mchezaji maarufu wa Chess wa Urusi, pia anahusika katika biashara ya mafuta na IS. Hata hivyo, hajalitaja jina la mchezaji huyo.

Katika mapambano dhidi ya IS, Rais Putin ametoa wito wa kuwepo ushirikiano zaidi wa kimataifa katika kupambana na ugaidi, akisema hawahitaji maazimio hewa ambayo yanafanyika bila ya kuwepo mshikamano, bali wanahitaji kuchukuliwa kwa hatua maalum. Kabla ya kuanza kutuhubia, Rais Putin alikutana na wajane wawili wa wanajeshi wa Urusi waliokufa katika kampeni za nchi hiyo nchini Syria.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov leo anatarajiwa kukutana na mwenzake wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, pembezoni mwa mkutano kuhusu usalama wa Ulaya unaofanyika Belgrade, Serbia, baada ya Putin kukataa kukutana na Erdogan pembezoni mwa mkutano wa kilele wa mazingira mjini Paris, siku ya Jumatatu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE
Mhariri:Yusuf Saumu