1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Putin atabakia na mamlaka mengi"

Maja Dreyer11 Desemba 2007

Mada ambayo inazingatiwa hasa magazetini ni kuchaguliwa kwa mrithi wa rais Putin wa Urusi.

https://p.dw.com/p/CaD3
Dmitry Medvedev (kushoto) na Vladimir PutinPicha: AP

“Sasa ni wazi, nani atakuwa rais mpya wa Urusi, yaani Dmitrij Medvedev, mtu wa karibu wa Putin.”


Ni maneno ya mhariri wa “Kölner Stadt-Anzeiger”. Akichambua zaidi matokeo yake, mhariri huyu anaendela hivi:


“Warusi wengi wako tayari kumchagua mrithi yeyote Putin atakayemteua na vyombo vya habari vinavyothibitiwa na serikali vitamsifu mgombea huyu hadi uchaguzi utakapofanyika. Lakini Urusi ina mustakabali gani chini ya Medvedev? Ataendelea kuwa kibaraka wa Putin au atajikomboa akishapanda kiti cha rais? Kwa hakika, Medvedev anaelekea njia hiyohiyo ya rais Putin.”


Tukiendelea na gazeti la “Frankfurter Allgemeine” tunasoma vifuatavyo:


“Rais Putin alimsaidia sana mwanasheria huyu Medvedev ambaye ni mdogo kwa miaka 13 kushinda Putin na anayetokea mjini mwake St. Petersberg. Medvedev basi anafahamu mfumo wa mamlaka wa rais Putin, hata amesaidia kuuendeleza. Naibu waziri mkuu huyu anajulikana kuwa mtu wa vitendo ambaye amejitenga na marafiki wa Putin wafanyakazi wa zamani wa idara za ujasusi. Kuna uhakika fulani lakini kwamba Medvedev atahakikisha mfumo wa Putin unaoendelea.”


Gazeti la “Badische Neueste Nachrichten” linalochapishwa mjini Karlsruhe linaandika hivi kuhusu matukio huko Urusi:


“Kwa kumteua Medvedev kama mrithi wake, Putin anabakia na mamlaka mengi. Mgombea huyu naibu waziri mkuu hana malengo yake binafsi. Kinyume na mshindani wake wa zamani, aliyekuwa waziri wa ulinzi Sergej Ivanov, Medvedev hata hana watu muhimu wanaomuunga mkono. Mbinu yake ya kushinda ni kuwa mwaminifu kabisa wa Putin.”


Hatimaye ni uchambuzi wa “Berliner Zeitung”. Gazeti limeandika:


“Kinacholengwa nchini Urusi si kurekebisha siasa, bali kuiendeleza. Ili kufanya hivi, wenye mamlaka wanahitaji sura mpya, lakini hawataki mtu mwenye mawazo mapya. Kwa hivyo, si shida kwamba mawazo ya Dmitrij Medvedev hayajulikani. Inasemekana kwamba ni mliberali kuliko wanasiasa wengine. Lakini tena, haijulikani nani pia alizungumziwa kuwa mgombea. Kwa hivyo, tumeingia awamu nyingine ya mchezo huu kuhusu siasa za Urusi na suali ni: Nani anatawala huko Moskow? Katika historia hakuna hata katibu mmoja mkuu wala raisi yeyote wa Urusi ambaye alijibu suali hili kamili.”