1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin aamrisha jeshi lake liondoke Syria

Yusra Buwayhid15 Machi 2016

Urusi imesema jeshi lake liliopo Syria linajitayarisha kuondoka na kurudi nyumbani kufuatia amri iliyotolewa na Rais wa Urusi Vladimir Putin, baada ya kuanza kwa mazungumzo ya amani ya mzozo wa Syria mjini Geneva.

https://p.dw.com/p/1IDCd
Syrien russische Kampfjets
Picha: picture alliance/dpa/Russian Defence Ministry

Taarifa hiyo imetolewa siku moja baada ya Rais Putin kutoa amri ya kuondoka kwa baadhi ya wanajeshi waliopo nchini Syria. Amri aliyoitoa siku yaliyoanza mazungumzo ya amani yanayofanyika mjini Geneva.

“Ushirikiano wa jeshi la Urusi pamoja na jeshi la Syria na vikosi vengine vya kizalendo, vimefanikiwa kuleta mabadiliko makubwa na ya kushangaza katika mapambano dhidi ya ugaidi wa kimataifa,” amesema Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Aidha Putin ameongeza matumaini yake ni kwamba kujiondoa kwa jeshi la Urusi itakuwa ni "ishara nzuri" kwa pande zote zinazopigana.

Kuanza kwa mazungumzo hayo kunampa Putin nafasi nzuri ya kutangaza kusitisha kampeni yake ya mashambulizi ya anga iliyoendelea kwa miezi mitano na nusu nchini humo na ambayo ililisaidia kwa kiasi kikubwa jeshi la Rais wa Syria Bashar al- Asaad kukamata baadhi ya maeneo muhimu nchini humo na kujiongezea nguvu kabla ya kuanza mazungumzo.

Russland Wladimir Putin
rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Reuters/S. Ilnitsky

Baadhi ya wanajeshi wa Urusi watasalia kuwepo

Hata hivyo Putin ameweka wazi baadhi ya wanajeshi wa Urusi watabakia katika kambi ya kijeshi ya eneo la Latakia pamoja na bandari ya Tartus nchini humo. Aidha Shirika la habari la Syria limemnukuu Rais Asaad akisema, Urusi itasitisha mashambulizi yake ya anga, lakini baadhi ya wanajeshi wake watabakia nchini humo. Ikulu ya Syria imesema viongozi hao wawili walizungumza kwa njia ya simu na kufikia aumuzi huwo.

Licha ya kuondoshwa kwa baadhi ya wanajeshi wa Urusi, jeshi la Syria limesema litaendelea na kampeni yake ya kuyashambulia makundi ya kigaidi, ya Dola la Kiislamu-IS pamoja na la Al-Nusra.

Aidha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakubaliana na uwamuzi uliyochukuliwa na Urusi wa kuanza kuondoa wanajeshi wake nchini Syria.

Mashambulizi yaliyodumu miezi mitano na nusu

Urusi ilianza mashambulizi ya anga nchi Syria mwezi Septemba kwa madai ya kutaka kuliondoa kundi la kigaidi linalojiita dola la kiisilamu IS linalodhibiti sehemu kubwa ya nchi hiyo, lakini kampeni hiyo ya kijeshi kwa kiasi kikubwa ilikuwa na lengo la kumsaidia Rais wa Syria Bashar al-Asaad.

Ingawa Urusi imeweza imeweza kwa kiasi kikubwa kuingilia kati mapigano yanayoendelea nchini Syria, wanadiplomasi wanasema hakuna hakika iwapo itaweza pia kumshinikiza Rais Asaad kukubali kufikia makubaliano yatakayoleta suluhu ya mgogoro huwo.

Katikaripoti yake kwa wanachama wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Steffan de Mistura amesema kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa Febuari 27, yanaweza kuvunjika kirahisi na kwa maana hiyo yanahitaji kulindwa.

Mazungumzo ya mjini Geneva, yaliyoitishwa na Umoja wa mataifa yalianza jana, ambayo ni siku iliyotimia miaka mitano tokea kuanza kwa mzozo wa Syria, ikiwa ni jitihada za hivi karibuni za kusitisha mapigano yaliyosababisha vifo vya zaidi watu 270,000 na kupelekea mamilioni wengine kupoteza mkaazi yao.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/ape

Mhariri: Grace Patricia Kabogo