POTSDAM : Mfumuko mpya wa madeni kwa Afrika | Habari za Ulimwengu | DW | 20.05.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

POTSDAM : Mfumuko mpya wa madeni kwa Afrika

Mawaziri wa fedha wa mataifa ya magharibi wameonya kwamba Afrika inaweza kukabiliwa na mfumuko mpya wa madeni iwapo hatua za ukopeshaji zisizowajibika zitaendelea.

Katika mkutano wa Kundi la Mataifa Manane yenye maendeleo makubwa ya viwanda duniani katika mji Postdam nchini Ujerumani waziri wa fedha wa Ujerumani Peer Steinbrück amesema hususan China imekuwa ikitowa mikopo nafuu kwa Afrika ambayo inaweza kutowa tishio kwa bara hilo.Amesema mikopo ya aina hiyo inakwenda kinyume na sera iliokubaliwa na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF na inaweza kuitumbukiza Afrika kwenye madeni mapya.

Hapo mwaka 2005 Kundi la Mataifa Manane lilikubali kusamehe madeni ya dola bilioni 60 iwapo mataifa yanayoendelea yataanza kupiga vita umaskini.

Pia katika mkutano huo pendekezo la Ujerumani la kutaka kuwepo kwa utaratibu wa maadili kusimamia sekta ya fedha za akiba ya kinga umekataliwa.

Serikali ya Ujerumani mara kwa mara imekuwa ikielezea wasi wasi wake kwamba ukuaji wa haraka katika sekta hiyo unaweza kudhoofisha mfumo mzima wa fedha duniani.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com