1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pompeo amewasili Kabul katika juhudu za kuokoa mkataba

Saleh Mwanamilongo
23 Machi 2020

Waziri wa mambo ya nje wa marekani Mike Pompeo amewasili mjini Kabul ilikukutana na viongozi wa nchi hiyo katika juhudu za kuokoa mkataba baina ya marekani na Wataliban.

https://p.dw.com/p/3Ztwl
Mike Pompeo waziri wa mambo ya nje wa Marekani na rais wa Afganistan Ashraf Ghani
Mike Pompeo waziri wa mambo ya nje wa Marekani na rais wa Afganistan Ashraf Ghani Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Harnik

Waziri wa mambo ya nje wa marekani Mike Pompeo amewasili mjini Kabul ilikukutana na viongozi wa nchi hiyo katika juhudu za kuokoa mkataba baina ya marekani na Wataliban,huku Afganistan ikikumbwa na mzozo wa kisiasa na ule wa ugonjwa wa Corona ambavyo vinatishia taratibu ya amani nchini humo.

Mike Pompeo ametarajiwa kukutana na rais Ashraf Ghani na aliyekuwa waziri mkuu wake ambaye ni kiongozi wa upinzani Abdullah Abdullah aliyejitangaza kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa Septemba mwaka uliopita, ambao ulikumbwa na kashfa za wizi wa kura.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani alipokelewa kwenye uwanja wa ndege wa Kabul na mjumbe wa Marekani kwa ajili ya mazungumzo na Taliban, Zalmay Khalilzad,mara baada ya kuwasili kwake. Ametarajiwa kuanzisha mikutano mjini humo kwanza na wanadiplomasia wa Marekani, pia na Ghani na Abdullah na baadhi ya viongozi wengine wa kisiasa wa Afganistan.

Ziara hiyo imekuja siku moja baada ya mazungumzo baina ya serikali ya Afghanistan na kundi la Tabilan kuhusu kubadilishana wafungwa, moja wapo ya kipengee muhimu cha taratibu ya amani nchini humo.

Taliban yataka wafungwa wake wote kuwachiliwa huru

Pande hizo mbili zimetofautiana kuhusu kuachiwa kwa wafungwa hao ambapo serikali inataka kuwaachia kwa awamu huku Taliban ikitaka wafungwa wote kuachiwa mara moja kama ilivyoafikiwa katika makubaliano na Marekani mjini Doha, Qatar mwezi uliopita.

Mkwamo huo umetishia kurejesha nyuma mchakato wa amani uliojadiliwa kwa umakini kama ilivyoainishwa katika makubaliano hayo yanayojumuisha kuondolewa kwa vikosi vya kijeshi vya kigeni kutoka Afghanistan baada ya zaidi ya miaka 18 ya mapigano.

Mjumbe maalumu wa Marekani nchini Afghanistan Zalmay Khalilzad amesema kuwa pande hizo mbili zilizungumza kwa zaidi ya muda wa masaa mawili kupitia mtandao wa Skype katika mkutano uliowezeshwa na Marekani na Qatar.

Khalizad aliongeza kuwa kila mtu anafahamu kwamba tishio la virusi vya corona linafanya suala hilo la wafungwa kuwa la dharura na kwamba pande hizo mbili zilielezea dhamira yao katika kupunguza ghasia, kufanya mazungumzo ndani ya Afghanistan na makubaliano makhsusi ya kusitisha kabisa mashambulizi.

Wapiganaji wa Taliban na raia wakishangilia makubaliano baina ya Taliban na Marekani
Wapiganaji wa Taliban na raia wakishangilia makubaliano baina ya Taliban na Marekani Picha: Getty Images/N. Shirzada

Makubaliano hayo yaliyotiwa saini na Khalilzad na afisa mmoja mkuu wa Taliban mnamo Februari 29 mjini Doha, yaliweka msingi wa kuhitimisha vita vya muda mrefu vya Marekani vilivyoanza baada ya shambulizi la kigaidi la Septemba 11 mwaka 2001.

Makubaliano hayo, yaliafikia kuachiliwa huru kwa wapiganaji wanaofikia elfu 5 wa Taliban wanaozuiliwa mjini Kabul na hadi wanachama elfu 1 wa vikosi vya jeshi la serikali walio mikononi mwa kundi hilo la wanamgambo.

Hatua hiyo ilipaswa kuchukuliwa kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo ya amani kati ya serikali ya Afghanistan ambayo haikuwa sehemu ya mazungumzo yaliyosababisha kupatikana kwa makubaliano ya Doha na Taliban ambayo awali yalikuwa yafanyike Machi 10.Awali serikali ya Afghanistan ilikataa mpangilio huo.

Serikali yailaumu Talibana kuendelea na mashambulizi

Inaripotiwa kuwa rais Ashraf Ghani alikasirishwa na sharti la kuachiwa kwa wafungwa na kusema ni serikali pekee iliyo na uwezo wa kuidhinisha hatua kama hiyo.

Hatimaye alikubali mpango huo wa kuachiwa kwa wafungwa lakini kwa awamu na kusema hili lingefanyika tu iwapo ghasia zingepunguzwa.

Msemaji wa baraza la kitaifa la usalama nchini Afghanistan Javid Faisal, amesema wanahitaji hakikisho kwamba hawatarejea katika vita.

Hata hivyo kundi la Taliban limesema kuwa liko tayari kwa awamu inayofuata ya mazungumzo ya amani lakini halitakutana na maafisa wakuu wa serikali hadi wakati wafungwa wao watakapoachiliwa huru.

Maafisa wa serikali wameripoti kuwa tangu kutiwa saini kwa makubaliano ya Doha, wanamgambo wametekeleza mashambulizi kadhaa. Wanamgambo waliovamia kituo cha polisi katika mkoa wa Kusini wa Zabul siku ya Ijumaa waliwauwa takriban maafisa 24 wa polisi na wanajeshi.