Polisi yatumia mabomu ya kutowa machozi Nairobi | Habari za Ulimwengu | DW | 03.01.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

Polisi yatumia mabomu ya kutowa machozi Nairobi

NAIROBI

Nchini Kenya polisi imefyetuwa mabomu ya kutowa machozi na kutumia mabomba ya maji kutawanya mamia ya waandamanaji wanaopinga kuchaguliwa tena kwa Rais Mwai Kibaki.

Polisi pia imefyetuwa risasi hewani kutawanya waandamanaji waliokuwa wakieleka katika mji mkuu huo wa Kenya Nairobi kuhudhuria maaandamano ya upinzani yaliopigwa marufuku na serikali.

Mama Wangari Mathai mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ametowa wito kwa viongozi mahasimu wa Kenya kukutana kutatuwa mzozo huo.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika John Kufour ambaye ni Rais wa Ghana alikuwa anatazamiwa kuwasili nchini Kenya leo hii kusaidia kusuluhisha mzozo uliozuka baada ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 300 nchini kote hata hivyo inaonekana kwamba kutokana na hali mbaya ya usalama ziara hiyo ya Kufour imefutwa.Kiongozi huyo alikuwa ashirikiane na Jumuiya ya Madola inayowakilishwa na kiongozi wa zamani wa Sierra Leone Ahmad Tejan Kabbah ambaye anaongoza kundi la waangalizi wa uchaguzi la Jumuiya ya Madola nchini humo. Askofu Mkuu wa Kianglikana Desmond Tutu wa Afrika Kusini na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel pia anashiriki katika juhudi za usuluhishi.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga ambaye anasema ameporwa ushindi wa uchaguzi wa mkuu wa Kenya na Kibaki amekuwa akin’gan’gania wito wake kwa watu milioni mmoja kuandamana leo hii kupinga ushindi wa Kibaki.

Wakati huo huo Rais Yoweri Museveni wa Uganda amekuwa kiongozi wa kwanza barani Afrika kumpongeza Kibaki kwa ushindi wa urais.

Kubakia kimya kwa takriban viongozi wote wa Afrika baada ya Kibaki kutangazwa mshindi kumeonyesha wasi wasi juu ya madai ya wizi wa kura katika uchaguzi huo uliofuatiwa na wiki nzima ya ghasia.

 • Tarehe 03.01.2008
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CjnB
 • Tarehe 03.01.2008
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CjnB

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com