1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi wa Ufaransa wakamata watu 19 katika msako

30 Machi 2012

Polisi wa Ufaransa leo wamefanya msako wa kuyatafuta makundi ya waislamu wenye itikadi kali na kuwakamata washukiwa 19. Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa ameapa kwamba msako utaendelea.

https://p.dw.com/p/14VAy
MSako wa polisi Ufaransa
MSako wa polisi UfaransaPicha: Reuters

Kamata kamata hiyo ilifanyika katika miji kadhaa, ukiwemo mji wa Toulouse ambapo wiki iliyopita, Mohammed Merah, aliyesababisha vifo vya watu saba, aliuwawa kwa kupigwa risasi na polisi. Rais Sarkozy wa Ufaransa ameeleza kwamba polisi walilenga kuwakamata watu wenye itikadi kali ya kiislamu na kwamba hali ya hofu iliyopo Ufaransa kwa wakati huu inaweza kufananishwa na hofu iliyotanda nchini Marekani baada ya mashambulizi ya kigaidi yaliofanyika tarehe 11 Septemba mwaka 2001.

Sarkozy aliendelea kusema kwamba operesheni ya kuwakamata washukiwa waliomo katika makundi yenye itikadi kali ya kiislamu, haihusiani tu na mauaji yaliyofanywa Toulouse, bali lengo ni kukabiliana na Uislamu wa itikadi kali kwa ujumla katika nchi nzima. Maafisa wa shirika la ujasusi la Ufaransa, wakishirikiana na polisi maalum wa kuzuia ugaidi, walifanya msako katika miji ya Toulouse, Nantes, Marseille, Lyon, Nice, Paris na katika maeneo mengine.

Watu waliohudhuria mazishi ya Mohammed Merah
Watu waliohudhuria mazishi ya Mohammed MerahPicha: dapd

Sarkozy: "Huu ni mwanzo tu"

Vyanzo vya habari vimeeleza kwamba miongoni mwa waliokamatwa ni Mohammed Achamlane, ambaye ni kiongozi wa kundi lenye msimamo mkali wa kiislamu linalojiita Forsane Alizza. Bunduki tatu aina ya kalashnikov, risasi aina ya Glock pamoja na guruneti zilikutwa nyumbani kwa mshukiwa huyo. Hadi leo hakuna ushahidi kwamba Mohammed Merah, aliyefanya mauaji katika miji ya Toulouse na Montauban, alikuwa mfuasi wa kundi hilo. Wiki chache zilizopita, kundi la Forsane Alizza lilipigwa marufuku baada ya waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa, Claude Guéant, kulishutumu kundi hilo kuwafundisha wafuasi wake namna ya kupigana kwa kutumia silaha.

Rais Sarkozy amesema kwamba huu ni mwanzo tu na kuongeza kwamba zitafuata operesheni zaidi kama iliyofanyika leo asubuhi na zitakazoufanya uongozi wa Ufaransa ufukuze baadhi ya watu kutoka nchini humo. Sarkozy aliutetea pia uamuzi wa nchi yake wa kuwazuia baadhi ya wahubiri wa kiislamu kuingia nchini humo, akisema kwamba hataki watu wanaopigia debe maadili yaliyo kinyume na yale ya Ufaransa kukaribishwa kuingia nchini humo. Aliongeza kwamba ni jukumu la serikali kuwahakikishia Wafaransa usalama. Wakati huo huo, viongozi wa Ufaransa wamewasihi wananchi wao kutoufananisha uislamu na ugaidi.

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa
Rais Nicolas Sarkozy wa UfaransaPicha: dapd

Mwandishi: Elizabeth Shoo/AFPE/APE/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman