1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Poland kuelekea Umoja wa Ulaya

Maja Dreyer23 Oktoba 2007

Wahiri wa magazeti hii leo wanabakia kwenye mada ya uchaguzi nchini Poland ambapo waziri mkuu, Jaroslaw Kaczynksi, atalazimika kuondoka madarakani. Mshindi ni mpinzani, Donald Tusk, na chama chake cha kiliberali. Wafuasi wake basi walimshangilia na wahariri wa magazeti ya hapa Ujerumani wanatumai nchi hiyo jirani na Ujerumani itabadilisha sera zake kuelekea Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/C7lF

Kwanza ni gazeti la “Tageszeitung” la mjini Berlin:

“Donald Tusk ni mwanasiasa anayefaa kabisa kuanza upya. Miaka miwili iliyopita alishindwa katika uchaguzi akilaumiwa kwamba anawapenda mno Wajerumani. Safari hii lakini, lawama hiyo haikumwathiri. Kwani, ndiyo, alikiri kuwa anawapenda Wajerumani, sawa na Wacheki, Waslovaki, Waingereza na Warusi.”

Gazeti la “Die Welt” linachambua makosa aliyoyafanya waziri mkuu aliyeshindwa Kaczynski. Limeandika:

“Jaroslaw Kaczynski wa mrengo wa kihafidhina na kizalendo angeweza kushinda rahisi. Hali ya Poland ni nzuri kama vile haijawahi kutoka katika karne tatu zilizopita. Lakini Kaczynski aliamini kwamba yeye si mwanasiasa pekee, bali pia ni mwanamapinduzi mwenye haki ya kutekeleza sheria kama anavyopenda bila ya kujali demokrasia.”

Gazeti la “Die Welt”. Mhariri wa “Kölnische Rundschau” anaonya kuwa ushindi wa upinzani pekee haumaanishi hali itaboreka. Ameandika:

“Sasa kuna matumaini kwamba chini ya Donald Tusk na sera zake za kiliberali kila kitu kitakuwa sawa. Soko liimarishwe na serikali ijiondoe. Sasa tunatumai tu kwamba rais Lech Kacynski hatamzuia Tusk kwa kutumia kura yake ya turufu. Ikiwa Tusk atashindwa kutekeleza mageuzi, Wapoland watapoteza kabisa imani juu ya demokrasia, soko huru au Umoja wa Ulaya.”

Na hatimaye tunasikia uchambuzi wa mhariri wa gazeti la kiuchumi la “Handelsblatt”:

“Polen itachukua muda kufika kabisa barani Ulaya na kusahau juu ya yale yaliyotokea katika historia. Sisi tunapaswa kuipa Poland muda huu na kuwa na subra. Hususan sisi Wajerumani ambao tulikuwa na mahusiano ya karibu katika historia na tutanufaika kutokana na Poland kujiunga na Umoja wa Ulaya. Huenda Donald Tusk kama waziri mkuu ataweza kuharakisha mambo. Angalau mazungumzo naye yatakuwa mazuri zaidi.”