1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Paslastina ukingoni mwa vita vya wenyewe kwa wenyewe

Oummilkheir13 Juni 2007

Hamas wawapa muda watumishi wa idara ya usalama wasalim amri kabla ya saa 12 jioni

https://p.dw.com/p/CB3e
Jengo la idara ya usalama laripuliwa
Jengo la idara ya usalama laripuliwaPicha: AP

Hali imepotoka moja kwa moja katika Ukanda wa Gaza ambako wafuasi wa Hamas wanaendelea kupigana na wale wa Fatah katika kinyang’anyiro cha kuania madaraka.Watu zaidi ya 58 wameshauwawa tangu mapigano hayo yaliporipuka June sabaa iliyopita.

Wapiganaji wa Hamas wameyazunguka makao makuu ya idara ya usalama mjini Gaza tangu asubuhi,wakiendelea na mapigano makali yaliyolengwa kuwatimua wanajeshi wa usalama,watiifu kwa chama cha Fatah cha rais Mahmoud Abbas.

Mapigano huko Gaza na hasa karibu na makao makuu ya vikosi vya usalama,yaliyoanza tangu leo alfajiri yameshagharimu maisha ya zaidi ya watu sabaa,katika wakati ambapo mtoto mmoja ameuwawa katika mapigano mengine ya wenyewe kwa wenyewe,katika mtaa mwengine wa Gaza.

Kwa mujibu wa mashahidi wanamgambo wa Hamas wamezizingira ofisi mbili za idara ya usalama katika mtaa wa Al Mashtal na kuzihujumu kwa makombora.

Risasi zimefyetuliwa kutoka pande zote mbili-Hamas na maafisa wa idara ya upelelezi waliojificha ndani ya jingo hilo.

Jumla ya watu 58 wamepoteza maisha yao tangu mapigano haya yaliporipuka June sabaa iliyopita.

Hamas ambao jana waliyateka makao makuu kadhaa pamoja na idara zinazomtii rais Mahmoud Abbas,wanaonyesha wamedhamiria kuumaliza mvutano naa Fatah kwa mtutu wa bunduki .

Jana usiku wajumbe wa kamati kuu ya chama cha Fatah walikutana Ramallah katika ukingo wa magharibi na kutishia mawaziri wa Fatah hawatoshiriki tena serikalini ikiwa mapigano hayatasita.

Ofisi ya rais wa Palastina inawatuhumu Hamas kutaka kufanya mapinduzi ili kuidhibiti Gaza na kuitumbukiza nchi katika janga la vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Na ofisi ya waziri mkuu Ismael Haniyeh inawashutumu,bila ya kuwataja kwa majina”watu wanaoshirikiana na adui” kwa lengo la kutaka kuipundua serikali ya umoja.”

Sauti zimeshaanza kupazwa kulaani mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kati ya wapalastina.Waziri wa habari,asieelemea upande wowote ,Mustapha Barghouti amesema:

“Cha hatari zaidi hapa ni pale utawala wa Palastina utakapovunjika ikiwa mapigano yataendelea.Ndio maanqa lengo la kila mmoja kwa sasa lingekua kusitisha mapigano na kurejea katika meza ya mazungumzo.”

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon amewatolea mwito wale wanaohusika na mzozo wa mashariki ya kati wamsaidie rais Mahmoud Abbas katika juhudi zake za kurejesha sheria na nidhamu.

Nae mkuu wa tume ya Misri iliosimamia makubaliano ya kuweka chini silaha,makubaliano yaliyovunjwa jumatatu iliyopita,amewatolea mwito wapalastina waandamane hii leo kudai silaha ziwekwe chini.

Waziri mkuu Ismael Hanniyeh na rais wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas,wote wawili wametoa mwito wa subira na kurejea katika meza ya majadiliano.

Lakini miito yote hiyo yaonyesha kupuuzwa na wafuasi wa pande hizo mbili wanaotuhumiana kutumikia masilahi ya Israel.Hivi punde Hamas wamewapa muda watumishi wa idara za usalama wasalim amri kabla ya saa 12 jioni.

Nchini Israel waziri mkuu Ehud Olmert amezungumzia madhara ya kimkoa pindi eneo zima la Gaza likidhibitiwa na Hamas.