1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pascal Lamy mkurugenzi wa WTO

1 Septemba 2009

Ameanza awamu ya pili ya miaka 4.

https://p.dw.com/p/JNFv

Pascal Lamy amechaguliwa tena kuwa Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Biashara duniani (WTO) na hii ni mara ya kwanza kutokea.Kuanzia jana septemba mosi, hali imebadilika.Kwani, tangu jana mfaransa huyo ameanza awamu yake ya pili kama mkurugenzi wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) kwa kipindi cha miaka 4 zaidi.Anaendelea kuwa hivyo ingawa mafanikio ya kipindi chake cha kwanza hayaridhishi.Tangu miaka mingi sasa mazungumzo ya Doha ya kurekebisha mfumo wa biashara ulimwenguni yamekwama.

Pascal Lamy katika awamu yake hii ya pili, anakabiliwa na kazi ngumu :Anabidi kuyakwamua mazungumzo ya Doha ,kwani yalipaswa kukamilishwa huko Cancun,Mexico 2003.Na licha ya majaribio kadhaa tangu miaka 6 iliopita, mazungumzo hayo bado yamenasa.Hatahivyo, Pascal Lamy hakukata bado tamaa kama asemavyo hapa -Kamishna huyu wa zamani wa biashara wa Umoja wa Ulaya:

"Naamini tumetoka mbali na sasa tumekaribia kufikia mwisho wa safari yetu."

Hiyo ndio risala ya Pascal Lamy kwa wanachama 153 wa Shirika la Biashara Ulimwenguni (WTO) mwishoni mwa Julai,mwaka huu.Mojawapo ya majukumu makubwa ya mkurugenzi huyu ni kupatanisha katika mazungumzo ya vikundi mbali mbali ili kufikia muwafaka.

Kwani unaweza kusema kuwa, kuna vikundi viwili vinavyohanikiza wakati huu katika shirika hilo la Biashara: Upande mmmoja, kuna mataifa ya kiviwanda kama Marekani,Umoja wa Ulaya au Japan. Zamani dola hizi zikiafikiana wenyewe kwa wenyewe katika mazungumzo haya.Ugomvi ukisuluhishwa kwenye vikao visivyo rasmi .Wanachama waliosalia katika duru hiyo, walibidi kuridhia walioamua hata ingawa ipo kanuni ya kubidi kuafikiana kwa sauti moja ndani ya shirika hilo.

Mchezo kama huo hauwzekani tena.Kwani, kuanzia miaka ya 1990, kundi la nchi changa na zile zilizoinukia kiuchumi, lilianza kujiandaa vyema.Na hasa dola 3 -Brazil,Afrika Kusini na India, zinapatana kwa nguvu na zinatumika kama waakilishi wa mataifa ya kusini mwa sayari hii.China kwa upande wake, imekuwa ikijiweka kando.

Sasa imekusudiwa mazungumzo hayo kuyaendeleza kandoni mwa mkutano wa kilele wa kundi la nchi 20 tajiri -G-20 huko Pittsburg,Marekani kuanzia Septemba 24-25.

Kumaliza mazungumzo ya Doha hivi sasa lingekuwa jambo la maana sana .Kwavile , biashara ya dunia tangu vita vya pili vya dunia imepanuka na kukua mfululizo, msukosuko wa uchumi ulimwenguni umesababisha sasa kuanguka mno kwa biashara hiyo.

.......Kwa muujibu wa taarifa za Shirika la Biashara Duniani (WTO), bidhaa zilizosafirishwa nje ulimwenguni mnamo miezi 3 ya kwanza ya mwaka huu, zilipungua kwa thuluthi-moja.Ikiwa ushuru wa forodha chini ya makubaliano mapya ya Shirika hili utapunguzwa,itawezekana kuutia jeki tangu uchumi hata biashara ya dunia .

Mwandishi:Beck,Johannes/Ali,Ramadhan

Mhariri:Abdul-Rahman