1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papandreou anusurika katika kura ya kuwa na imani

5 Novemba 2011

Waziri mkuu wa Ugiriki Geirge Papandreou ameshinda kura ya kuwa na imani na utawala wake , iliyopigwa bungeni mapema leo Jumamosi baada ya kuahidi kuanzisha mazungumzo ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

https://p.dw.com/p/135V8
Waziri mkuu wa Ugiriki George Papandreou akizungumza bungeni Jumamosi.Picha: dapd

Waziri mkuu wa Ugiriki George Papandreou ameshinda kura ya kuwa na imani na utawala wake iliyopigwa bungeni mapema leo Jumamosi baada ya kuahidi kuanzisha mazungumzo ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa katika nchi hiyo inayokumbwa na mizozo. Papandreou aliitisha kura hiyo akiangaliwa kwa tahadhari na masoko ya fedha pamoja na viongozi wenzake wa Ulaya, licha ya ushindi mwembamba alioupata kwa chama chake cha kisoshalist pamoja na uasi miongoni mwa viongozi wa chama hicho.

Jumla ya wabunge 153 miongoni mwa wabunge 298 waliokuwapo bungeni waliidhinisha hoja hiyo, amesema spika wa bunge huku akishangiliwa.

Matokeo hayo yanaweka uwiano huku kukiwa na hali mbaya ya wasi wasi wakati kila mbunge akipiga kura ama kukubali ama kukataa, huku kambi zote zikikaribiana hadi mwishoni.

Kura hiyo inaifanya Ugiriki kuwa na uwezekano wa kutekeleza masharti ya mpango mkubwa wa uokozi wa umoja wa Ulaya wenye lengo la kuiweka nchi hiyo ambayo iko ukingoni mwa kufilisika kupata uhai na ni suala litakalosifiwa kote katika bara la Ulaya.

Akitoa wito wa kuunda serikali ya mseto ya umoja wa kitaifa ili kutekeleza mpango huo wa Ulaya , waziri mkuu huyo ambaye alikuwa katika mbinyo mkali ameliambia bunge kuwa yuko tayari kwa serikali hiyo ya umoja wa kitaifa.

Muda mfupi kabla ya wabunge kuanza kupiga kura , Papandreou alitangaza kuwa atamtaka rais wa Ugiriki kumpa mamlaka ya kuanza mazungumzo juu ya kuunda serikali kama hiyo. Uaminifu na uungaji mkono mkubwa unahitajika , ameliambia bunge kabla ya upigaji kura kuanza. Mabadiliko ambayo yanahitajika ni ya kihistoria na yanahitaji ushiriki wa wananchi.

Amepuuzia miito ya wapinzani kutaka uchaguzi na mapema , akisema kuwa uchaguzi wa aina hiyo utakuwa maafa . Haikufahamika mara moja iwapo atakuwa kiongozi wa serikali hiyo wakati itakapoundwa.

Griechenland Finanzkrise Opposition Antonis Samaras Partei Neue Demokratie
Kiongozi wa upinzani wa chama cha kihafidhina Antonis Samaras anadai uchaguzi na mapema.Picha: dapd

Lakini , katika ishara ya wazi kuwa atajiweka kando , amesema kuwa hataweka mapenzi yake mbele ya kazi ya uokozi wa taifa hilo.

Sina nia ya kung'ang'ania madaraka , kitu cha mwisho ambacho nakihitaji ni iwapo nitachaguliwa tena. Iwapo kwa matendo yangu naweza kutoa ujumbe kuwa sisi sio maadui, hapo nitakuwa nimetoa mchango mkubwa kwa nchi hii katika muda wa miaka 30 ambayo nimekuwa katika shughuli za uongozi, amesema.

Desturi za familia yangu haziniruhusu kufanya kitu ambacho ni tofauti, amesema Papandreou , ambaye baba yake na babu yake pia walikuwa viongozi.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre

Mhariri : Sudi Mnette.