1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis atoa wito wa amani duniani

Sekione Kitojo
1 Aprili 2018

Katika  siku  ya  furaha kuu  kwa Wakristo,  kiongozi  wa  kanisa Katoliki  papa  Francis  katika  ujumbe  wake  wa  Jumapili  ya Pasaka  alitoa  wito wa  amani  katika  dunia  ambayo  imegubikwa na  vita  na  mizozo.

https://p.dw.com/p/2vL69
Vatikan Papst Franziskus Urbi et Orbi
Picha: Reuters/S. Rellandini

Akianza  na  nchi anayopenda  kutoa  wito  wa  amani na  inayokabiliwa  na  vita  vya  muda mrefu  ya Syria,"  aliendelea  katika  eneo  lote  la  mashariki  ya kati, rasi  ya  Korea  na  sehemu za  Afrika zilizoathirika  na  'njaa, mizozo isiyokwisha  na  ugaidi."

Francis aliakisi  mtazamo  wake  katika  nguvu  ya  imani ya  msingi ya  Ukristo  kwamba  Yesu  aliamka  kutoka  mautini  baada  ya kuteswa  msalabani , katika  ujumbe  wake  wa  kila  mwaka  wa Pasaka  unaojulikana  kama "Urbi et Orbi"  ama  "kwa  mji  na  dunia" unaotolewa  katika  kibaraza cha  kanisa  la  Mtakatifu  Petro Basilica katika  uwanja  wa  kanisa  hilo  uliojaa  watu pomoni.

Vatikan Papst Franziskus Ostermesse auf dem Petersplatz
Umati wa watu waliohudhuria misa ya Pasaka katika kanisa la Mtakatifu Petro mjini Vatican (01.04.2018)Picha: picture-alliance/AP Photo/C. Peri

Kiongozi  huyo  wa  kidini amesema  ujumbe  wa  ufufuo  unatoa matumaini  katika dunia "inayokabiliwa  na  matukio  mengi  ya kutokuwa  na  sheria  na  matumizi  ya  nguvu."

"Unazaa  matunda ya  matumaini  na  utu  ambako  kuna udhalilishaji na  kutengwa, njaa  na  ukosefu wa  ajira; kule  ambako  kuna wahamiaji  na  wakimbizi, ambao  kila  mara  wanakataliwa  na utamaduni  wa ubadhirifu katika  siku hizi, na wahanga  wa  biashara ya  madawa  ya  kulevywa , biashara  ya  kusafirisha  watu  kwa  njia haramu na  njia  za  utumwa wa  kisasa, " Papa  alisema.

Ametoa  wito   wa "kumalizwa  kwa  haraka " mauaji   nchini  Syria, akisisitiza  kwamba  misaada ipelekwe  haraka  kwa  wanaoihitaji nchini  humo  na  kutoa  wito  wa "hali inayokubalika  ya  kurejea  na wale  waliokimbia makaazi yao."

Vatikan Papst Franziskus Urbi et Orbi
Papa Francis akipungia umma uliojitokeza katika kumbukumbu ya sikukuu ya pasakaPicha: picture-alliance/AP Photo/G. Borgia

Papa ataka  maridhiano Israel na  Palestina

Papa  pia  amehimiza  maridhiano nchini  Israel  na  ana  matumaini  kwamba  "kuheshimiana kutakuwapo  badala  ya  utengano"  nchini  Yemen  na  katika  eneo lote  la  Mashariki  ya  Kati.

Akigeukia barani  Asia, Francis  ana  matumaini  kwamba mazungumzo  yanayoendelea  yanaweza  kuleta  amani  katika  rasi ya  Korea, na  kuhimiza " wale ambao wanahusika  moja  kwa  moja kuchagukua  hatua  za  busara  na utu kuhimiza  kila  jambo  jema kwa  watu  wa  Korea.

Kwa upande  wa  Ukraine, papa  amehimiza hatua  zaidi  kuchukuliwa kuleta  umoja  katika  taifa  hilo  lililogawika. Pia  ametoa  wito  wa amani  katika  Sudan kusini na  Jamhuri  ya  kidemokrasi  ya  Congo, akiitaka dunia  kutowasahau  wahanga  wa  mizozo  hiyo, hususan watoto.

"Iwapo  hakuna  mshimano  na  wote  wale waliolazimika  kukimbia mataifa  yao  ya  asili  na  ukosefu wa  vitu  muhimu  vya kuwawezesha  kuishi," Papa  amesema  mara  kadhaa  amekuwa msitari  wa  mbele  katika  utetezi  wa  wahamiaji na  wakimbizi.

Venezuela Caracas Protest
Maandamano nchini VenezuelaPicha: Reuters/C. G. Rawlins

Kiongozi  wa  kwanza  wa kanisa  hilo  kutoka Amerika ya kusini amedokeza  hususan  matatizo  nchini  Venezuela, akieleza matumaini  kwa  nchi  hiyo kwamba "itapata  njia  ya  haki, amani na utu ili  kuwa  haraka  juu  ya  mzozo  wa  kisiasa  na  kiutu  ambao unaikumba  nchi hiyo."

Mapema, mamia  kwa  maelfu  ya  waumini  walipitia  ukaguzi  mkali wa  usalama  kuingia  katika  uwanja  wa  Mtakatifu Petro kuhudhuria sala  ya  Jumapili  ya  Pasaka iliyoongozwa  na  Papa,  iliyofuatiwa na  ujumbe  wa "Urbi et  Orbi".

Mwandishi: Sekione  Kitojo / ape

Mhariri: John Juma