1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis aanza ziara nchini Misri

28 Aprili 2017

Kiongozi wa Kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis ameanza ziara nchini Misri, katika juhudi za kuhimiza maelewano kati ya Wakristu na Waislamu na kuepusha ghasia zinazofanywa kwa kutumia jina la Mungu.

https://p.dw.com/p/2c68q
Ägypten Papst Franziskus in Kairo | mit Abdel Fattah al-Sisi
Papa Francis akisalimiana na Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri mjini CairoPicha: Reuters/The Egyptian Presidency

Mara tu baada ya kuwasili mjini Cairo mchana wa leo, Papa Francis amepokelewa na Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi kwa heshima za kijeshi, huku makasisi wakijipanga mstari kumsalimia. Baadaye ametembelea chuo kikuu maarufu cha Kiislamu cha Al-Azhar, ambako amefanya mazungumzo na Mufti Mkuu Ahmed al-Tayeb, yaliyoelezewa kama yenye kukamilisha mchakato wa kuboresha mahusiano kati ya Wakatoliki na Waislamu wa madhehebu ya Sunni. Akizungumza na waandishi wa habari ndani ya ndege kabla ya kutua mjini Cairo, Papa Francis amesema ziara yake ya masaa 27 itakuwa ya kusajiisha umoja na udugu. Ujumbe huo pia ndio alioutoa kwa watu wa Misri, kabla ya kufunga safari kuizuru nchi yao.

''Kwa moyo wenye furaha na shukrani nitaitembelea nchi yenu, ambayo ni kitovu cha ustaarabu na zawadi wa Mto Nile, nchi ya jua na ukaribu, ambako maaskofu na manabii waliishi, na ambako Mungu mwenye rehema na uwezo, aliitoa sauti yake'', alisema Papa Francis na kuongeza, ''Ninayo furaha ya kweli kuja kama rafiki, na kama mjumbe wa amani katika nchi ambayo miaka 2000 iliyopita, iliipa hifadhi familia takatifu iliyokuwa ikikimbia kitisho cha mfalme Herod.''

Mjadala kati ya waislamu na wakristo

Ägypten Besuch vom Papst Franziskus in Kairo
Ulinzi uliimarishwa mjini Cairo wakati wa ziara ya PapaPicha: Reuters/Egypt TV/A. Abdallah Dalsh

Katika ziara yake hiyo fupi, Papa Francis atakutana kwa pamoja na viongozi wa Kiislamu na wa Kikristu, kabla ya kulitembelea kanisa lililoshambuliwa kwa mabomu mwezi Desemba mwaka jana. Watu 29 walipoteza maisha katika shambulio hilo. Shambulio jingine kwenye kanisa la Koptiki mwezi huu wa Aprili liliuwa waumini 45.

Makanisa yote nchini Misri yamewekewa ulinzi wa ziada, kwa hofu kuwa mashambulizi mengine yanaweza kufanywa wakati huu wa ziara ya Papa Francis. Licha ya wasiwasi kuhusu usalama lakini, Papa Francis anatarajiwa  kutumia gari la kawaida tu katika shughuli zake.

Wakati ya ziara yake hii nchini Misri, Papa Francis atahutubia mkutano wa kimataifa kuhusu amani ambao umeandaliwa na chuo cha al-Azhar, ambacho ni kituo cha maarufu cha elimu kwa zaidi ya miaka 1000, chenye msikiti wenye historia ya fahari kubwa.

Kukosoa makosa ya Papa Benedikt wa XVI

Francis ni Papa wa kwanza kuitembelea Misri tangu ziara nyingine ya kihistoria iliyofanywa nchini humo na Papa John Paul wa II mwaka 2000. Uhusiano kati ya Misri na makao makuu ya Kanisa Katoliki uliingia doa enzi za Papa Benedikt wa 16, ambaye kufuatia shambulizi jingine kwenye kanisa la Koptik mwaka 2006 alitoa kauli iliyochukuliwa kama yenye kuunganishi dini ya Islamu na ghasia, kauli iliyokosolewa na chuo cha Al-Azhar kama uingiliaji wa mambo ya ndani ya Misri.

Wakristu wa madhehebu ya Koptik ni asilimia kumi ya wakazi wote milioni 92 wa Misri, na wamekuwa wakilengwa na mashambulizi ya mara kwa mara. Rais wa sasa wa Misri, japo anachukuliwa kama mtu anayetawala kwa mkono wa chuma amekuwa rafiki wa wakristu walio wachache nchini humo, na mwaka 2015 alikuwa rais wa kwanza wa Misri kushiriki katika ibada ya Krismasi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, ape

Mhariri: Mohammed Khelef