1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Benedikt wa 16 atangaza kujiuzulu

11 Februari 2013

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Ulimwenguni,Papa Benedikt wa 16, ametangaza atajiuzulu Februari 28, tukio la aina ya pekee katika historia ya Kanisa hilo, na hivyo kuuduwaza ulimwengu mzima.

https://p.dw.com/p/17c9o
Papa Benedikt wa 16 akitangaza uamuzi wa kujiuzuluPicha: Reuters

"Ndugu zangu, nimekuiteni ili kukuarifuni kuhusu uamuzi muhimu kwa mustakbali wa kanisa letu. Baada ya kutafakari mara kadhaa moyo wangu mbele ya Mungu, nimeamua kwa uhakika kwamba nguvu zangu, kutokana na umri wangu mkubwa, haziniruhusu niendeshe jukumu langu kikamilifu."

Uamuzi huo wa kiongozi wa 265 wa Kanisa Katoliki ulimwenguni na papa wa kwanza mwenye asili ya Ujerumani tangu karne ya 11, umewashangaza mpaka washauri wake wa karibu sana, amesema msemaji wa Vatican, Federico Lombardi.

Lombardi amesema uamuzi huo umewaduwaza kwa sababu Papa Benedikt wa 16 si mgonjwa na wala hakumbwi na shinikizo la aina yoyote.

Lombardi ameongeza kusema kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki ulimwenguni ataendelea na jukumu lake hadi hadi tarehe ya kujiuzulu itakapowadia na kwamba baadae atasalia kwa muda katika jumba la msimu wa kiangazi la mapapa huko Castelgandolfo kabla ya kuhamia katika jumba moja la ibada mjini Roma.

Ujerumani yaheshimu uamuzi wa Papa Benedikt wa 16

Beginn Kabinettssitzung Angela Merkel Steffen Seibert CDU Bundeskanzleramt Berlin
Kansela Angela Merkel na msemaji wa serikali yake Steffen SeibertPicha: dapd

Mkuu wa makadinali huko Vatikan, Angelo Sodano, ameuzungumzia uamuzi huo kama "raadi" katika mbingu zilizotakata.

Serikali ya Ujerumani imeelezea jinsi ilivyoshitushwa na uamuzi huo wa Papa Benedikt wa 16. Hata hivyo, Kansela Angela Merkel amesema anaheshimu kwa dhati uamuzi huo, kama anavyosema msemaji wa serikali kuu ya Ujerumani, Steffen Seibert:"Serikali kuu ya Ujerumani ina heshma kubwa mbele ya Baba Mtakatifu, jukumu lake na yote aliyofanya kwa ajili ya Kanisa Katoliki. Ni miaka takriban minane sasa tangu aliongoze Kanisa hilo. Sababu za uamuzi wake, bila ya kutaka kujua kwa nini, ni za kuheshimiwa na kuthaminiwa pamoja na kushukuriwa kwa kuliongoza kanisa hilo ulimwenguni kwa muda wote huu wa miaka minane."

Rais Francoise Hollande wa Ufaransa ameuita uamuzi huo kuwa wa kuheshimika.Sifa na shukurani zimetolewa kutoka kila pembe ya dunia ,toka kwa wachamungu mpaka wanasiasa.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki ulimwenguni atasherehekea miaka 86 ya kuzaliwa kwake tarehe 16 Aprili mwaka huu. Alichaguliwa kuliongoza kanisa hilo tarehe 19 Aprili mwaka 2005.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef