1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Benedikt wa 16 amaliza ziara yake ya siku nne nchini Ufaransa

Hamidou, Oumilkher15 Septemba 2008

Ziara ya kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni yasifiwa nchini Ufaransa

https://p.dw.com/p/FIgM
Papa Benedikt wa 16 anasali katika kanisa dogo la hospitali moja huko LourdesPicha: AP


Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni,Papa Benedikt wa 16 amerejea Roma leo mchana baada ya   kuongoza misa kwaajili ya walemavu,mwishoni mwa ziara ya  siku nne mijini Paris na Lourdes .



Kabla ya kuondoka toka mji huo wa kusini magharibi unaotembelewa kila mwaka na malaki ya waumini wa kikatoliki,kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni alihutubia ,katika uwanja wa ndege wa Tarbes mbele ya maelefu ya waumini wakiwemo walemavu zaidi ya elfu mbili. Waziri mkuu Francois Fillon nae pia alihudhuria misa hiyo.


"Kuna mapambano ambayo hatuwezi kushinda bila ya msaada wa Mungu" amesema Papa Benedikt wa 16,aliyewabariki pia wagonjwa kumi.


Katika hotuba yake,kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni,Papa Benedikt wa16 amemshukuru pia rais Nicholas Sarkozy na viongozi wa Ufaransa ambao anasema tunanukuu:"wamefanya kila liwezekanalo kufanikisha ziara hii ya toba."


Waziri mkuu amezungumzia "mwamko wa umma uliosababishwa na ziara hii ya kwanza ya Pape."


"Kuanzia misa katika kanisa kuu la Notre Dame mjini Paris,kupitia  l'Esplanade des Invalides hadi kufikia Lourdes,moyo wako wa upendo umemulika nyoyo za umati wa watu waliojaa furaha na wanaosikiliza kwa makini risala yako"-amesema waziri mkuu wa Ufaransa Francois Fillon.



Mnamo siku nne za ziara yake nchini Ufaransa,ya kwanza kufanya tangu alipochaguliwa kuongoza kanisa katoliki ulimwenguni miaka mitatu iliyopita,Papa Benedikt wa 16 alizungmzia mada tete inayohusu mtindo wa kutoingilia kati kanisa katika mambo ya kisiasa nchini Ufaransa.Papa Benedikt wa 16 amehimiza "watafakari upya kuhusu nafasi ya kanisa nchini humo."Amewatolea mwito wakuu wa kanisa nchini Ufaransa  wasiregeze kamba  linapohusika suala la talaka na ndowa za watu walioachana na kutetea haja ya misa kuongozwa kama zamani kwa lugha ya kilatini.


Jana kiongozi huyo wa kanisa katoliki aliongoza misa iliyohudhuriwa na zaidi ya waumini laki moja na nusu kutoka kila pembe ya dunia,kuadhimisha miaka 150 tangu  bikira Maria alipomjilia msichana mdogo Bernadette Soubirou karibu na pango la Massabielle.


Alipokua njiani kuelekea Lourdes Papa Benedikt 16 alisema:



"Siku kuu ya mtakatifu Bernadette ndio siku niliyozaliwa.Kwa sababu hiyo pia nnajihisi niko karibu nae sana msichana huyo mdogo."


Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni amelitaja eneo hilo kua "nuru inayomulika nyoyo za wale ambao bado wanasita sita katika kufuata njia ya Mungu".


 Baadhi ya vyombo vya habari vya Ufaransa vimeisifu ziara ya kiongozi wa kanisa katoliki na kusoma imefana.


Mwenyekiti wa baraza la maaskofu la Ufaransa Andre Vingt-Trois ameshukuria kuona ziara ya Papa imewavutia pia vijana na kulipatia sura mpya kanisa nchini Ufaransa.