1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa akosoa hali ya kambi za wahamiaji nchini Libya

Admin.WagnerD8 Julai 2020

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis amevilinganisha vituo vya wakimbizi huko Libya na kambi za mateso, na kusema ulimwengu unafichwa hali halisi ya mateso yanayowakabili watu wanaoishi katika kambi hizo. 

https://p.dw.com/p/3ez2Z
Vatikan | Papst Franziskus während Ostermesse im Petersdom
Picha: Getty Images/AFP/A. Solaro

Papa Francis ambaye hapo awali aliwahi kutoa wito wa kutaka kambi hizo za Libya zifungwe, ameyasema hayo wakati wa Misa ya kuadhimisha kumbukumbu ya miaka saba ya safari yake ya Kisiwa cha Italia cha Lampedusa, mahali wanaposhukia wahamiaji wengi wanaofanya safari hatari ya kuvuka bahari ya Mediterania wakitokea kaskazini mwa Afrika.

Akikumbuka aliyoyashuhudiwa wakati wa safari yake hiyo ya mwaka 2013, Francis amesema alisikiliza simulizi za mateso kutoka kwa wahamiaji hao kupitia kwa mkalimani, lakini alikuja kutambua baada ya kurudi Vatican kwamba mkalimani huyo alimtafsiria sehemu tu ya walichokisema wahamiaji hao.

Francis amesema hivyo ndivyo ilivyo mara nyingi, ulimwengu unaelezwa kwa mukhtasari tu kuhusu vita na mateso yanayotendwa huko nchini Libya.

"Vita vinatisha, tunajua hivyo, lakini huwezi kufikiria mateso watu wanayoishi nayo huko, katika kambi zinazowaweka kizuizini. Na watu hao walikuja na matumaini wakati wakivuka bahari," amesema Papa Francis 

Papa Francis aliwahi kutembelea maeneo wanakofikia wahamiaji 

Papst Frankziskus Lampedusa Italien
Papa Francis alipotembelea kisiwa cha Lampedusa mwaka 2013Picha: picture-alliance/dpa/Osservatore Romano

Na leo hii imetimia miaka saba tangu safari hiyo ya Francis ambayo ilikuwa ya kwanza nje ya mji mkuu wa Rome kama Papa na kukutana na wahamiaji waliowasili kasiwa hicho cha Lampedusa kupitia boti za wanaovusha watu kinyume na sheria kutoka Libya.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, maelfu ya wakimbizi na wahamiaji wanawekwa katika vituo 20 vya uzuiaji vinavyotambuliwa rasmi. Kambi nyinginezo zinaendeshwa na makundi ya wanamgambo, na kambi nyingi zisizojulikana idadi yake zinaendeshwa na wafanyabiashara haramu ya kusafirisha binadamu.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yamerikodi visa vya ubakaji, mateso na unyanyasaji mwingine katika vituo hivyo vya Libya vya kuhifadhi wahamiaji. Kuna madai pia ya wahamiaji wanaotafuta hifadhi kurejeshwa katika kambi hizo baada ya kuokolewa na walinzi wa pwani ya Libya.

Italia pamoja na Umoja wa Ulaya, wenye lengo la kuzuia uingiaji mkubwa wa wahamiaji barani Ulaya, wametumia mamilioni ya yuro kuongeza uwezo wa walinzi wa pwani ya Libya wa kupiga doria mipakani mwake. Na makundi ya kutetea haki za binadamu yanadai kwamba hatua hiyo imewafanya kuwa washiriki katika uhalifu huo unaotendwa kwenye vituo vya wahamiaji nchini Libya.

Mara kwa mara Francis amekuwa akionyesha mshikamano na wahamiaji wanaovuka bahari ya Mediterania na kuomboleza wale ambao wamepoteza maisha katika safari hizo. Na amekuwa pia akirudia matamshi ya kuyalaani mataifa tajiri yanayokataa kuwakaribisha wakimbizi.

Mwandishi: Yusra Buwayhid

Mhariri: Iddi Ssessanga