1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pakistan yakabiliwa na ongezeko la idadi ya watu

2 Agosti 2007

Mabadiliko ya hali ya hewa duniani yanalaumiwa kuwa yanasababishwa na ongezeko la watu. Lakini Dr Shaheen Rafi Khan wa taasisi ya SDPI, inayoshughulika na utafiti nchini Pakistan anasisitiza kwamba mabadiliko hayo yanasababishwa pia na jinsi jamii zinavyo ishi pamoja na matumizi ya vyanzo asilia.

https://p.dw.com/p/CHju
Rais Perves Musharaf wa Pakistan
Rais Perves Musharaf wa PakistanPicha: PA/dpa

Dr. Shaheen Rafi Khan mtalaamu wa maswala ya hali ya hewa anasisitiza kwamba hali halisi inategemea zaidi na binadamu anavyoishi na pia matumizi yake ya vyanzo asilia mbali na idadi ya watu, anasema uharibifu wa hali ya hewa unasababishwa na mtawanyiko wa gesi chafu kutoka eneo moja hadi jingine kwa mfano kutoka kaskazini na kupokewa na upande wa kusini ambao ndio unaopata athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Ameitaja India ambayo inakabiliwa na ongezeko la haraka la watu na wakati huo huo nchi hiyo ni miongoni mwa nchi zinazo shuhudia kukuwa kwa uchumi wake katika kiwango cha haraka mno.

Huku jamii katika nchi masikini zinapojitahidi kujikimu kimaisha hatari ya kuyaharibu mazingira nayo inaongezeka. Malengo ya baadae yanapuuzwa kwa sababu za mahitaji ya sasa.

Matumizi ya miti kwa wingi kwa ajili ya kuni, uharibifu wa vyanzo vya maji na uharibifu wa ardhi kutokana na malisho kwa wanyama kupita kiasi pamoja na uvuaji wa samaki kupindukia yote haya ni mambo yanayoendelea kwa kasi katika nchi masikini.

Katika bara Asia sababu nyingine kubwa inayochangia uharibifu wa hali ya hewa ni ukuaji wa haraka wa viwanda katika nchi za India na China unaosababisha utoaji wa gesi chafukwa wingi.

Lakini licha ya yote hayo ongezeko la watu duniani ndio chanzo hasa cha mabadiliko ya hali ya hewa.

Katika utafiti wake Dr Shaheen Rafi Khan anasema kama dunia ingelikuwa na takriban watu milioni 100 tu basi idadi hiyo ingeweza kugharamia mahitaji yake ya nishati kulingana na mfumo wa maisha na athari dhidi ya sayari yetu ingekuwa ndogo mno.

Dr. Khan amesema kwamba kufikia mwaka 2050 bara la Asia litawajibika kukidhi mahitaji ya kimazingira ya takriban raia bilioni 2.4, idadi hiyo ilikuwa sawa na idadi ya watu wote duniani katika mwaka 1950.

Idadi ya watu duniani inatarajiwa kuongezeka kwa kiwango cha asilimia 40 kufikia mwaka huo wa 2050.

Nchini Pakistan mpango wa kupanga uzazi haufui dafu kama inavyohitajika kwani hatua hiyo haipendelewi zaidi na watu wengi, wanasiasa na viongozi wa dini ambao wanatarajiwa kutoa mchango wao mkubwa katika hili hawatimizi wajibu wao ipasavyo.

Katika jamii nyingi nchini Pakistan swala la dawa za kupanga uzazi ni swala ambalo halizugnumzwi waziwazi na familia.

Kwa mfano elimu kwa jamii za vijijini ni kitendawili ambcho hakina jibu jamii bado ziko gizani,….. namnukulu Dr. Khan, hakujengwi mashule na badala yake tunakuza vikosi vya majeshi…Misho wa kumnukulu

Hali hiyo imeisababishia Pakistan kuwa na idadi kubwa ya jamii changa vijiji ambazo zina uwezo wa kupata watoto kwa wingi na hazina uwezo wa kufikia kwa urahisi huduma za kupanga uzazi.

Mwanasayansi Dr Shaheen Rafi Khan anawahimiza viongozi wa Pakistan watoe mchango wao zaidi katika kulishughulikia swala la ongezeko la watu ili kukabiliana vilivyo na uharibifu wa hali ya hewa.