1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ouattara ataka amani na maridhiano Cote d'Ivoire

12 Aprili 2011

Nchini Cote d'Ivoire,Jumuia ya kimataifa imeonesha nia ya kufanya kazi na serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na Alassane Ouatarra, ambaye amelitaka jeshi lake kutolipiza kisasi Katika kuwakamata wafuasi wa Gbagbo.

https://p.dw.com/p/10rph
Alassane OuattaraPicha: AP

Ikiwa ni siku moja tu baada ya kukamatwa kwa Laurent Gbagbo ambaye alikuwa aking'ang'ania madarakani, Umoja wa Ulaya umetangaza kushirikiana na serikali ya Cote d'Ivoire kuweza kuondoa vikwazo vyote vilivyowekewa nchi hiyo, vikiwa na lengo la kumshinikiza Gbagbo aliyekuwa akigoma kuondoka madarakani, kujiuzulu.

Mkuu wa kitengo kinachohusika na masuala ya Diplomasia, katika Umoja wa Ulaya ambacho kinatoa huduma kwa nchi za Afrika Nicholas Westcott amesema, watashauriana na serikali ya Ouattara juu ya vikwazo vya kiuchumi vilivyobaki dhidi ya makampuni ya Cote d'Ivoire.

kufuatia ombi la Rais Ouattara alilolitoa wiki iliyopita, Umoja wa Ulaya umeondoa vikwazo tayari katika bandari ya Abidjan na ile ya San Pedro na pia kampuni ya mafuta.

Ouattara ataka amani:

Akizungumza kupitia televisheni ya nchi hiyo ikiwa ni hotuba yake ya kwanza kuitoa toka alipokamatwa mpinzani wake kisiasa Laurent Gbagbo hapo jana, Allasane Outtara, ambaye pia aliita mwanzo wa enzi mpya ya matumaini kwa raia wa nchi hiyo, ametangaza pia hatua za kisheria dhidi ya mpinzani wake huyo na watu wake.

Elfenbeinküste Laurent Gbagbo Verhaftung
Laurent Gbagbo, baada ya kukamatwa janaPicha: dapd

Aidha amesisitiza kuwa hatua zote zinachukuliwa kuhakikisha wanalindwa kufuatia tukio zima la kukamatwa kwake hapo jana baada ya miezi minne ya machafuko nchini humo.

Kituo cha Televisheni cha Rais Ouattara kimemuonesha Gbagbo jana akiwa ndani anayoshikiliwa pamoja na wasaidizi wake kadhaa, huku akionekana amechoka, lakini bila ya madhara yoyote.

Jumuia ya kimataifa yapongeza:

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameipongeza ahadi iliyotolewa na Ouattara ya kuunda Tume ya maridhiano na ukweli kufuatilia madai ya mauaji ya watu wengi na uhalifu mwingine uliofanywa na pande zote mbili katika mzozo huo.

Ban Ki Moon Pressekonferenz New York
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moonPicha: Picture Alliance/Photoshot

Ban Ki moon alifahamisha kuwa pia kwamba Bwana Gbagbo kwa sasa anashikiliwa na majeshi ya Ouattara na kwamba visa zaidi vya umwagaji damu vitaepukwa.

Umoja wa mataifa unazaidi ya wanajeshi elfu tisa na polisi nchini Cote d'Ivoire na kwamba vikosi hivyo vitaendelea kukaa nchini humo ili kusaidia kurejesha utawala wa sheria.

Tayari viongozi mbalimbali duniani wametia kauli yao kuhusiana na kukamatwa kwa Rais Gbagbo na hali nchini humo, ambapo Rais Barack Obama wa Marekani amepongeza na kusema kuwa kazi ya kuijenga upya nchi hiyo na maridhiano yanapaswa kuanza sasa.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle kwa upande wake alikuwa na haya.

Waziri wa mambo ya Nchi za Nje wa Ufaransa, Alain Juppe amesema kukamatwa kwa Gbagbo ni habari nzuri kwa demokrasia barani Afrika.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri: Mohammed Abdulrahman