1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

OPEC kutobadili sera za uzalishaji mafuta licha ya kuporomoka kwa bei hizo

Mohamed Dahman10 Septemba 2008

Saudi Arabia yaridhika na kushuka kwa hivi karibuni kwa bei za mafuta na imeonekana kuwa haiko katika utashi wa kubadili sera ya uzalishaji mafuta ya Shirika la Nchi Zenye Kusafirisha Mafuta kwa Wingi Duniani OPEC.

https://p.dw.com/p/FEyT
Makao makuu ya OPEC mjini Vienna Austria.Picha: AP

Ipo inafanya mkutano wake leo hii mjini Vienne Austria wakati bei ya mafuta ghafi ikishuka kufikia takriban dola mia kwa pipa.

Waziri wa mafuta wa Saudi Arabia Ali al- Nuaimi amesema kabla ya kuanza kwa mkutano huo wa sera wa OPEC mjini Vienna kwamba wamefanya juhudi kubwa sana tokea mwezi wa Juni kuzifikisha bei mahala zilipo hivi sasa na kwamba anafikiri kila kitu kiko katika uwiano.

Waziri huyo pia amedokeza kwamba mkutano huo wa nchi wanachama 13 zinazosafirisha nje mafuta kwa wingi duniani OPEC utaamuwa kuendelea kufanya uzalishaji kutoyumba licha ya kuwepo kwa wasi wasi wa kuanguka haraka kwa bei za mafuta.

Wakati Saudi Arabia ikitowa theluthi moja ya uzalishaji wa nchi wanachama wa OPEC maoni yao mara nyingi hupitishwa katika mikutano ya mawaziri na hiyo tamko hilo la al Naimi inaonyesha kwamba mawaziri hao wataendelea kushikilia hali iliopo sasa ya uzalishaji wa mafuta.

Kauli yake inaonekana kuzima wito wa kupunguzwa kwa uzalishaji wa mafuta uliotolewa hapo jana na waziri wa mafuta wa Iran Gholam Nozari aliesema kwamba usambazaji wa mafuta umepindukia katika soko.

Venezuela ambayo kwa kawaida huunga mkono bei ya juu ya mafuta leo hii waziri wake wa mafuta Rafael D. Ramirez amesema hakuna haja ya dharura kupunguza uzalishaji wa mafuta.

Saudi Arabia ambalo ni taifa linalozalisha kwa wingi kabisa mafuta ghafi duniani na linaloonekana kama kiongozi wa shirika la OPEC imekuwa chini ya shinikizo zito la Marekani na washirika wake wengine kutokana na kuongezeka kwa hivi karibuni kwa bei za mafuta kulikovunja rekodi.

Nchi hiyo imekubali hapo mwezi wa Mei na Juni kuzalisha mapipa ziada ya mafuta 500,000 kwa siku kusaidia kushusha bei za mafuta zilizokuwa zikipanda ovyo ambazo zilifikia juu ya dola 147 hapo mwezi wa Julai lakini hivi sasa ziko hatarini kushuka tena kufikia kiwango cha chini ya dola mia moja kwa pipa.

Lakini baadhi ya wachambuzi wanaamini nchi wanachama wa OPEC zinaweza kuamuwa upunguzaji mkubwa wa mafuta wakati mahitaji ya mafuta yakipunguwa jambo ambalo litafanikishwa kwa kupunguza uzalishaji wa mafuta wa kupindukia kuvuka fungu lao rasmi la uzalishaji bila ya kutangaza rasmi mabadiliko hayo ya sera.

Shirika la Ushauri Elekezi la Nishati NFP Energy lenye makao yake mjini Washington Marekani limebaini kwamba OPEC kimsingi limekubali kupunguza uzalishaji wa mafuta kutoka viwango vya hivi sasa kupindukia malengo rasmi ya uzalishaji kwa mapipa kama 500,000 kwa siku.

Bara la Ulaya litaendelea kutegemea kuagizia mafuta kutoka nje kwa sababu uzalishaji wa mafuta barani humo unaendelea kupunguwa.

Kwa mtizamo wa Martin Zagler mtaalamu wa masuala ya fedha na mwangalizi wa shughuli za OPEC.

hiyo ina maana kwamba bei ya mafuta haitoyumba na hususan haitoteremka chini.

Hivi sasa inaaminika kwamba OPEC inazalisha takriban mapipa ya mafuta milioni moja kwa siku zaidi ya kiwango chake rasmi cha milioni 29.67 Saudi Arabia ikiwa ndio yenye kuzalisha sehemu kubwa sana ya ziada hiyo.

Iran imekuwa ikiongoza wito wa nchi wanachama wa OPEC kutimiza mafungu yao ya uzalishaji kutakakopelekea kupunguwa kwa mafuta katika masoko.

Venezuela,Libya na Algeria zote zimeelezea wasi wasi wao juu ya kuwapo kwa mafuta ya kupindukia katika soko kutokana na kudhoofika kwa uchumi duniani.