1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Olmert ziarani Marekani atajadili mradi wa kinuklia wa Iran

P.Martin10 Novemba 2006

Waziri mkuu Ehud Olmert wa Israel,siku ya Jumapili ataelekea Washington.Bila ya shaka atakaribishwa kwa ukunjufu na mshirika mkuu wa Israel baada ya kiongozi huyo kutoa miito ya kuchukuliwa hatua kali kuhusika na mradi wa kinuklia wa adui mkuu-Iran.

https://p.dw.com/p/CHLA
Ehud Olmert akipokewa na George W.Bush wakati wa ziara yake ya mwezi Mei nchini Marekani
Ehud Olmert akipokewa na George W.Bush wakati wa ziara yake ya mwezi Mei nchini MarekaniPicha: AP

Miezi sita baada ya Olmert kupokewa kwa sherehe na rais George W.Bush,pale aliposhinda uchaguzi, kwa ahadi ya kuipanga upya mipaka ya Israel, mkutano wa kilele utakaofanywa Novemba 13 umeelezwa na Jerusalem kama ni mkutano wa kazi kuhusu Iran. Kwa mujibu wa msemaji wa Olmert Bibi Miri Eisin,mada kuu katika ajenda ni suala la Iran na hilo si siri.Ikiungwa mkono na Marekani,Israel inasema kuwa vikwazo ni lazima, baada ya serikali ya Teheran kukataa kusitisha mpango wake wa kurutubisha madini ya Uranium. Israel,Marekani na nchi nyingi za Ulaya zinasema mpango huo wa Iran unaficha mradi wa kutengeneza silaha za kinuklia kwa siri.Iran lakini inashikilia kuwa mradi huo ni kwa matumizi ya amani.

Israel,inayodhaniwa na wengi,kama ni dola pekee lenye silaha za kinuklia katika Mashariki ya Kati-hata ikiwa haikutangazwa-huichukulia Iran kama ni adui wake mkuu.Hapo,Israel inakumbusha miito ya rais Mahmoud Ahmedinejad wa Iran kuwa dola la Wayahudi lifutiliwe mbali kwenye ramani.

Wakati wa mkutano wao wa mwezi Mei,Bush alimuhakikishia Olmert kuwa “Marekani itaisaidia Israel ikiwa kutafanywa shambulio lo lote lile dhidi ya Israel.”

Serikali ya Teheran ikiendelea kukataa miito ya kimataifa kuwa isitishe mradi wake wa kinuklia kurutubisha uranium,sasa ndio kitisho cha Iran kimepangwa juu kabisa katika ajenda ya Israel. Wakati huo huo,Israel imekariri kuwa mradi wa kinuklia wa Iran si kitisho kwa Israel peke yake bali ni kwa kanda nzima.Ikaongezea kuwa ni hatari pia kwa zile nchi zinazoweza kufikiwa na makombora ya masafa ya mbali aina ya Shahab-3,ambayo hivi karibuni yalijaribiwa na Iran.Kwa mujibu wa mwana diplomasia mmoja wa zamani wa Israel mjini Washington,Olmert na Bush watajadiliana njia za kuizuia Iran kupata silaha za kinuklia.Lakini afisa wa Kimarekani wa ngazi ya juu amesema “Israel haitolenga vituo vya kinuklia vya Iran kwa sababu Israel imesema kuwa hilo ni tatizo la ulimwengu mzima.Israel inaelewa kuwa njia pekee ya kuutenzua mgogoro huo wa kinuklia ni kupitia utaratibu wa kidiplomasia.”

Bush na Olmert vile vile wanatarajiwa kuzungumzia uwezekano wa kuanzishwa tena majadiliano ya amani kati ya Waisraeli na Wapalestina.Majadiliano hayo yatafanywa chini ya wingu la mauaji ya Wapalestina 18 yaliofanywa na vikosi vya Israel siku ya Jumatano kwenye Ukanda wa Gaza.Israel imeeleza masikitiko yake na kusema kuwa kosa lilitokea katika shambulio hilo.Jumuiya ya kimataifa imelaani vikali shambulio hilo na hata Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana katika kikao cha dharura kulijadili suala hilo.