1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Olmert na Abbas wakubali kuendelea na majadiliano

P.Martin12 Machi 2007

Waziri mkuu wa Israel,Ehud Olmert na Rais wa Wapalestina,Mahmoud Abbas,wamekutana mjini Jerusalem kujadiliana kuhusu serikali ya umoja wa kitaifa ya Wapalestina,inayotazamiwa kuundwa.

https://p.dw.com/p/CHIQ
Waziri Mkuu Olmert na Rais Abbas kabla ya mkutano wao mjini Jerusalem
Waziri Mkuu Olmert na Rais Abbas kabla ya mkutano wao mjini JerusalemPicha: AP

Huu ni mkutano wa pili kufanywa kati ya Olmert na Abbas katika kipindi cha mwezi mmoja.Majadiliano yao yalifanywa nyumbani kwa kiongozi wa Israel,mjini Jerusalem na yalidumu saa mbili. Licha ya kwamba hakuna matokeo thabiti yaliyopatikana,viongozi hao walikubali kuendelea na majadiliano yao.Hapo awali,katika kikao cha baraza la mawaziri la Israel,Olmert alisema anaunga mkono mradi wa amani wa Saudi Arabia wa mwaka 2002.Kuambatana na mradi huo,uhusiano wa nchi za Kiarabu pamoja na Israel utarekebishwa, ikiwa Israel itarudi nyuma kwenye mipaka ya mwaka 1967 na itakubali kutafuta suluhisho la pamoja kuhusu tatizo la wakimbizi wa Kipalestina.

Akiendelea,Waziri mkuu Olmert alisema,ikiwa mkutano wa kilele wa Umoja wa nchi za Kiarabu utakaofanywa mjini Riyadh mwisho wa mwezi huu, utasisitiza sehemu muhimu za mradi huo,basi nafasi ya kuendelea na utaratibu wa amani itakuwa bora.

Kwa mara nyingine tena,Olmert alimsisitizia Rais wa Wapalestina Abbas kuwa Israel itaisusa serikali ya Wapalestina inayotazamiwa kuundwa, ikiwa serikali hiyo mpya haitoitambua Israel na mikataba ya amani iliyokuwepo na haitotangaza kuachilia mbali matumizi ya nguvu.

Wakati huo huo,naibu waziri mkuu wa Israel,Shimon Peres amesema,msingi wa kuanzishwa majadiliano ya kidiplomasia ni ule mpango wa amani ujulikanao kama “Road Map” pamoja na masharti ya kundi la pande nne-yaani Marekani,Umoja wa Ulaya,Umoja wa Mataifa na Urussi.

Lakini chama cha Wapalestina cha Hamas chenye msimamo mkali,hadi hivi sasa kimekataa kutambua rasmi taifa la Israel.Kwa upande mwingine ripoti zinasema kuwa kiongozi wa chama cha Kipalestina cha Fatah,Mahmoud Abbas anataka kumuomba Waziri Mkuu Olmert aitazame serikali ya muungano itakayoundwa na vyama vya Hamas na Fatah kama ni hatua ya maendeleo.Baraza la mawaziri la serikali ya Hamas na Fatah linatazamiwa kutangazwa katika muda wa siku chache zijazo.