1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Odinga amtaka Rais Kibaki akubali kushindwa

30 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/Ci3B

NAIROBI.Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Amolo Odinga amemtaka Rais Mwai Kibaki kukubali kushindwa katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliyofanyika Alhamisi wiki hii.

Vinginevyo Odinga ambaye ni kiongozi wa chama cha ODM amesema kuwa tume ya uchaguzi ianze upya zoezi la kuhesabu kura.

Kiongozi huyo amemtuhumu Rais Kibaki kwa wizi wa kura na kulielezea zoezi zima la kuhesabu kura kuwa lenye hitilafu kubwa.

Uhesabuji kura umesitishwa wakati ambapo tume ya uchaguzi nchini humo inapitia upya baadhi ya matokeo.

Kuchelewa kutolewa kwa matokeo hayo kumepelekea ghasia ambapo inaarifiwa ya kwamba watu watatu wameuawa katika ghasia hizo.

Raila alikuwa akiongoza kwa wingi mkubwa wa kura dhidi ya Rais Kibaki. Lakini katika matokeo yaliyotangazwa jana na tume ya uchaguzi, mwanya wa kura hizo ulipungua ambapo Raila alikuwa mbele kwa kura elfu 38 dhidi ya Rais Kibaki.

Mapema vyama vyote viwili kile cha Rais Kibaki cha PNU na ODM vilidai kupata ushindi katika uchaguzi huo.

Mapya kuhusiana na uchaguzi huo utayapata mara baada ya taarifa hii ya habari.