1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama, Castro wasifu uhusiano mpya baina yao

Iddi22 Machi 2016

Marais wa Marekani na Cuba wameahidi kuweka kando tofauti zao na kuendeleza kile rais wa Marekani alichokitaja kuwa "siku mpya" katika uhusiano baina ya majirani hao waliohasimiana kwa zaidi ya miongoni mitano.

https://p.dw.com/p/1IHJM
Rais wa Cuba Raul Castro na mgeni wake Barack Obama mjini Havana.
Rais wa Cuba Raul Castro na mgeni wake Barack Obama mjini Havana.Picha: Reuters/J. Ernst

Baada ya mazungumzo kati ya Obama na Castro - ya kwanza kati ya marais hao kwenye ardhi ya Cuba na ya tatu tangu nchi hizo zianze kujongeleana, Obama alisema yeye na Castro walikuwa na mjadala wa wazi kuhusu haki za binaadamu na vile vile maeneo mengine ya ushirikiano, akisisitiza hata hivyo kuwa uhusiano huo utaimarika zaidi ikiwa Cuba itaboresha rekodi yake ya haki za binaadamu

"Marekani inatambua hatua zilizopigwa na Cuba kama taifa, mafanikio yake makubwa katika elimu na huduma za afya, na pengine muhimu zaidi nasisitiza kuwa mustakabali wa Cuba hautaamuliwa na Marekani au taifa lolote lingine," alisema Obama na kuongeza kuwa Cuba ni nchi huru inayojivunia nafasi yake, na hatma ya Cuba itaamuliwa na Wacuba wenyewe.

Rais Raul Castro akimuongoza mgeni wake kukagua gwaride la kijeshi lililoandaliwa kwa ajili yake.
Rais Raul Castro akimuongoza mgeni wake kukagua gwaride la kijeshi lililoandaliwa kwa ajili yake.Picha: Reuters/C.Barria

Katika mkutano wao ambao wakati mwigine ulipambwa na vichekesho na wakati mwingine hasirahasira -- na ambao katika hali isiyokuwa ya kawaida ulirushwa moja kwa moja na vituo vya habari vya serikali -- Castro alikiri kuwa zipo tofauti za kimsingi kuhusu masuala ya haki za binaadamu na vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani dhidi ya nchi yake.

Alitoa wito wa kuondolewa kwa vikwazo hivyo, lakini alikataa kukiri kuwa serikali yake inawashikilia wafungwa wa kisiasa. "Nipe orodha sasa hivi ya wafungwa wa kisiasa na nitawaachia. Wafungwa gani wa kisiasa? Nipe jina, au majina, au tukimaliza mkutano nipatie orodha ya hao wafungwa na kama kweli wapo, wataachiwa kabla hakujakucha," alisema Castro.

Mabadiliko makubwa yanaonekana

Licha ya hayo lakini, ukweli kwamba mkutano huo wa pamoja ulifanyika katika Kasri la Mapinduzi la Havana, baada ya viongozi hao kukutana kwa saa mbili, ulidhirisha kuwa mabadiliko makubwa yametokea. Leo Jumanne Obama atapeleka ujumbe wake moja kwa moja kwa Wacuba, katika hotuba inayotarajiwa kutangazwa moja kwa moja nchini kote.

Msaidizi wa Obama kuhusu sera ya kigeni Ben Rhodes, alisema hotuba hiyo ni muhimu sana kwa sababu ndiyo fursa pekee katika ziara hii kurudi nyuma na kuzungumza moja kwa moja na watu wa Cuba. Rhodes aliashiria kuwa Obama atagusia uhusiano wa zamani, fursa zinazokuja na ufunguaji huu mpya pamoja na matarajio ya baadae.

Kukamatwa kwa wapinzani wakati wa ziara ya Obama kumetilia mkazo suala la haki za binaadamu nchini Cuba.
Kukamatwa kwa wapinzani wakati wa ziara ya Obama kumetilia mkazo suala la haki za binaadamu nchini Cuba.Picha: Getty Images/AFP/A. Roque

"Wakati urekebishaji ukiendelea, na kuna idadi kubwa ya watu wanaotembelea hapa na vyombo vya habari vikikiangazia kisiwa hiki, unaona watu wakijieleza, na hilo ni jambo zuri, na hiyo ndiyo maana ya kufungua milango kwa ulimwengu," alisema Rhodes katika mkutano na waandishi wa habari uliyofanyika mjini Havana.

Obama atakutana pia na wapinzani wa Cuba Jumanne na kutazama mechi ya mchezo wa besiboli pamoja na mwenyeji wake, kati ya klabu ya Marekani ya Tampa Bay na timu ya taifa ya Cuba, na atakutana na viongozi wa kiraia katika ubalozi wa Marekani mjini Havana kabla ya kuendelea na safari yake nchini Argentina, kwa ziara ya siku mbili.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe

Mhariri: Josephat Nyiro Charo