1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama awaunga mkono majirani wa China mgogoro wa maeneo

Admin.WagnerD28 Aprili 2014

Rais Barack Obama wa Marekani yuko nchini Ufilipino, kituo cha mwisho cha ziara yake barani Asia, ambayo inalenga kuonyesha mshikamano kati ya Marekani na kanda hiyo, wakati wa mzozo baina ya China na majirani zake.

https://p.dw.com/p/1BpOh
Rais Barack Obama akisalimiana na rais wa Ufulipino Benigno Aquino baada ya kuwasili mjini Manila siku ya Jumatatu.
Rais Barack Obama akisalimiana na rais wa Ufulipino Benigno Aquino baada ya kuwasili mjini Manila siku ya Jumatatu.Picha: Reuters

Rais Obama aliwasili Ufilipino akitokea Malaysia na kuwasili kwake kumekuja saa chache baada ya Waziri wa ulinzi wa Ufilipino Voltaire Gazmin na Balozi wa Marekani Philip Goldberg kusaini mktaba wa miaka kumi wa kuimarisha ushirikiano wa ulinzi, ambao unairuhusu Marekani kuweko kijeshi nchini humo.

Mara tu baada ya kuwasili rais Obama alikwenda moja kwa moja kwenye kasri la Rais la Malacanang kwa mazungumzo na Rais Benigno Aquino kuhusu juhudi za kuimarisha ushirikiano wa ulinzi na usalama pamoja na uchumi kati ya nchi zao mbili.

Picha hii inamuonyesha rais Obama akiwa na mfalme ya Malaysia Abdul Halim wa Kedah (wa tatu kulia) na waziri mkuu Najibu Razak (wa nne kulia) wakati wakimkaribisha katika viwanja vya bunge mjini Kuala Lumpur siku ya Jumamosi.
Picha hii inamuonyesha rais Obama akiwa na mfalme ya Malaysia Abdul Halim wa Kedah (wa tatu kulia) na waziri mkuu Najibu Razak (wa nne kulia) wakati wakimkaribisha katika viwanja vya bunge mjini Kuala Lumpur siku ya Jumamosi.Picha: JIM WATSON/AFP/Getty Images

Migogoro kati ya China na majirani zake

Baadae rais Aquino alisema wamekubaliana kwamba migogoro ya maeneo itatuliwe kwa njia ya amani. Ufilipino imetaka utatuzi wa kimataifa katika mgogoro wake na China ambayo inadai kiasi ya 90 asili mia ya eneo la kusini mwa bahari ya China. China pia ina mgogoro na Brunei, Malaysia, Vietnam na Taiwan.

Obama kwa upande wake alisema lengo la marekani si kuidhibiti China, hata hivyo aliunga mkono juhudi za Ufilipino kusaka usuluhisho wa kimataifa.

Mkataba wa ulinzi na Ufilipino unayaruhusu majeshi ya Marekani kutumia kambi za kijeshi nchini Ufilipino, kujenga vituo vipya na kuweka manuwari na ndege za kivita kisiwani humo, ikiwa ni miaka 20 baada ya vituo vya jeshi la majini na anga vya Marekani kufungwa nchini humo .

Migogoro itatuliwe kwa amani

Ziara ya Obama pamoja na mkataba mpya wa kijeshi, ni mambo yanayojiri katika wakati ambao Ufilipino imo katika jitihada za kulinda ardhi yake dhidi ya madai na vitendo vya uchokozi vya China.

Katika ziara yake hii ya siku nne barani Asia ambayo imemchukuwa pia hadi Japan, Korea Kusini na Malaysia, Obama amesisitiza juu ya haja ya kuitatuwa migogoro ya maeneo kwa amani bila ya vitisho au uvamizi.Katika mji mkuu wa Malaysia Kuala Lumpur jana, Obama alisema mataifa yote lazima yaheshimu sheria za kimataifa.

Raos Obama akiwahutubia wanajeshi wa Marekani walioko nchini Korea Kusini.
Raos Obama akiwahutubia wanajeshi wa Marekani walioko nchini Korea Kusini.Picha: Kim Min-Hee - Pool/Getty Images

Wachambuzi wanasema mkataba wa ulinzi kati ya Marekani na Ufilipino utakuwa na athari mchanganyiko kwa Ufilipino, ambayo iliwahi kuipa Marekani Kambi kubwa kabisa ya jeshi la majini na anga, nje ya Amerika kaskazini kwa zaidi ya miaka 80, kabla ya baraza la Seneti kupiga kura mwaka 1992 ,kutorefusha mkataba uliokuwepo.

Mkurugenzi mkuu wa taasisi inayohusika na amani, machafuko na ugaidi Rommel Banlaoi, anasema mkataba huo una umuhimu wa kijeshi kwa kuwa unaimarisha ushirikiano wa kijeshi baina ya nchi hizo mbili. Lakini anasema kuna hatari zake, kwani Ufilipino itageuka lengo la maadui wa Marekani kama vile magaidi na hivyo kitisho dhidi ya Marekani kitageuka kitisho dhidi ya Ufilipino.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, Reuters, AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga.