1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama awafariji wakaazi wa Newtown

17 Desemba 2012

Rais wa Marekani Barack Obama ameahidi kutumia mamlaka yake yote kuhakikisha kuwa mikasa ya mauwaji yanayotokana na mashambulizi ya kiholela ya risasi haitokei tena.

https://p.dw.com/p/173de
US-Präsident Barack Obama spricht auf der Trauerfeier für die Opfer des Amoklaufs von Newtown (Foto: dpa)
USA, Newtown, Obama, Trauerfeier, Gedenkfeier, Amoklauf, Massaker, Kinder, GrundschulePicha: picture-alliance/dpa

Akizungumza katika mkesha wa maombolezii mjini Newtown ya watu 26 waliouawa katika shule moja ya msingi wakiwemo watoto 20, Obama amesema Marekani haifanyi vya kutosha katika kuwalinda watoto wake, na akaahidi kwamba katika wiki zijazo, ataanzisha juhudi za kupunguza mashambulizi kama hayo nchini humo.

Lazima kufanywe mabadiliko

Rais Obama amesema matukio ya mauwaji ya mashambulizi ya risasi hayawezi tena kuvumiliwa na ni lazima yafikie kikomo. Na kwa kutimiliza hilo, ni lazima pawepo mabadiliko. Rais huyo wa Marekani ameeleza mapenzi yake na maombi ya taifa kwa jumla kwa familia za wahanga wa mauwaji hayo, akisema Wamarekani wote wanasimama pamoja nao katika kuomboleza vifo hivi vya kikatili. Rais Obama ametoa wito wa dharura kwa Wamarekani kufanya kila wawezalo kuzuia kutokea tena mikasa isiyo na idadi ya ufyatuwaji risasi ambayo imeitia hofu nchi hiyo. Tangu kuchaguliwa kuwa rais, Obama ameshuhudia matukio manne makuu ya mauwaji ya kiholela kupitia risasi, lakini kumekuwa na visa vingine vidogo vilivyotokea katikati ya matukio hayo.

Biwi la simanzi bado limetanda katika mji wa Newtown, Connecticut
Biwi la simanzi bado limetanda katika mji wa Newtown, ConnecticutPicha: Reuters

Hakuna sheria inayoweza kuangamiza maovu duniani

Obama amekiri kwamba hakuna sheria yoyote inayoweza kutokomeza uovu duniani au kuzuia kila aina ya mauwaji katika jamii, lakini akadokeza kwamba atatafuta ufumbuzi wa suala hilo. Awali, maafisa walimtambua rasmi Adam Lanza, mwenye umri wa miaka 20, kuwa ndiye aliyefanya shambulizi hilo, wakithibitisha kwamba alimpiga risasi mamake mara kadhaa kichwani katika nyumba walimoishi, kabla ya kuelekea katika shule hiyo yake ya zamani na kufanya kitendo hicho cha kinyama. Polisi imesema Lanza alitumia bunduki ya mamake aina ya bushmaster 223 kuwauwa watu 26 shuleni humo, ikiwa ni pamoja na watoto 20 wenye kati ya umri wa miaka sita na saba, kabla ya kujiuwa na bastola wakati polisi walipowasili shuleni humo huku ving'ora vya magari vikilia.

Mamia wamehudhuria mkesha wa maombi ya wahanga wa mauwaji
Mamia wamehudhuria mkesha wa maombi ya wahanga wa mauwajiPicha: dapd

Waombolezaji waliohudhuria ibada hiyo iliyofanyika katika shule ambako kulitokea mkasa huo ya Sandy Hook, wametiririkwa na machozi wakati rais alipokuwa akiyasoma majina ya kila mmoja aliyeuawa katika shambulizi hilo siku ya Ijumaa. Mazishi ya wawili kati ya watoto 20 waliouawa katika mkasa huo yatafanywa leo. Wakati huo huo, shule kote Marekani zinafunguliwa tena hii leo huku watoto waliojawa hofu wakijiuliza ni kwa nini wenzao wakauliwa kinyama katika jimbo la Connecticut, na kama wako salama dhidi ya tukio jingine kama hilo

Mauwaji yazusha mjadala

Mauaji hayo yameamsha upya mjadala juu ya udhibiti wa silaha katika nchi ambapo utamaduni wa kumiliki silaha umeshamiri na kuna ushawishi mkuwa wa kupigia debe umilikaji wa silaha, jambo ambalo limewakatisha tamaa wanasiasa wengi kufanya jitihada zozote zile kubwa za kushughulikia tatizo la kumiliki silaha kwa urahisi. Meya wa mji wa New York Michael Bloomberg ambaye anaongoza muungano wa mameya katika suala la sera ya silaha amesema hapo Ijumaa kwamba Rais Obama wa chama cha Demokrat anapaswa kuchukuwa hatua licha ya upinzani kutoka chama cha Republikan ambacho kinalidhibiti Baraza la Wawakilishi la bunge la Marekani. Bloomberg amesema katika taarifa " Tumeyasikia madoido ya kusema kabla.Hatukushuhudia uongozi sio kutoka Ikulu wala kutoka bungeni. Jambo hilo halina budi kukomeshwa leo hii."

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri :Hamidou Oummilkheir