Obama atembelea ′Ground Zero′ | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.05.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Obama atembelea 'Ground Zero'

Rais Barack Obama amefanya ziara ya kumbukumbu katika eneo yalipokuwa majengo maarufu ya 'Twin Towers' mjini New York, siku chache baada ya kuuwawa Osama bin Laden anayeaminika kuandaa mashambulizi ya Septemba 11, 2001.

Rais Barack Obama akiwafariji maafisa wa zimamoto

Rais Barack Obama akiwafariji maafisa wa zimamoto

Katika kumbukumbu, Rais Obama aliweka shada la maua katika eneo la 'Ground Zero' kabla ya kuamkiana na jamaa za watu waliouwawa katika shambulio linalodaiwa kufanwa na wafuasi wa itikadi kali wa Al Qaeda katika majengo ya World Trade Center, pamoja na wizara ya ulinzi, Pentagon miaka 10 iliyopita.

Rais Obama amefanya ziara hiyo ambayo ni ya kwanza tangu alipochaguliwa kuwa rais wa Marekani, pasi na kutoa hotuba na alinyamaza kimya kwa muda baada ya kuweka shada hilo la maua.

Awali alizungumza katika jengo la wazima moto ambapo maafisa 15 waliuwawa walipokuwa wakipambana na moto wa shambulio hilo, na alisema kuwa ni tukio ambalo haliwezi kusahaulika.

'Ninatumai kuwa inawapa nyote utulivu kujuwa kuwa wakati kikosi kilipochukuwa hatua za hatari kwenda Pakistan, kilitambua kuwa kinafanya hivyo kwa ajili ya mauaji yaliotekelezwa hapa, kilifanya hivyo kwa ajili ya ndugu zenu waliofariki.' Rais Obama alisema.

Obama kukutana na makomando waliomuua Osama

Rais Barack Obama akikutana na wazimamoto wa New York

Rais Barack Obama akikutana na wazimamoto wa New York

Hivi leo, Rais Obama anatarajiwa kuwatembelea makomando waliofanikiwa kumuua Bin Laden nchini Pakistan. Makomando hao walioivamia nyumba ya Osama mjini Abbottabad, wanasemekana kutoka kwenye kikosi kijulikanacho kama 'Team Six', kikosi cha wasomi kilichotoka kwenye kikosi cha maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi - SEAL.

Uvamizi huo umesababisha jeshi la Pakistan kuitaka Marekani ipunguze wanajeshi wake nchini humo. Hii ni baada ya kuzuka maswali kuhusu jinsi gani Bin Laden alifanikiwa kupata hifadhi karibu na kambi ya jeshi. Mkuu wa Jeshi wa Pakistan, Jenerali Ashfaq Kayani, ametishia kuzingatia upya ushirikiano iwapo patakuwepo uvamizi mwingine wa Marekani.

Hata hivyo, Pakistan, ambayo ni mshirika wa karibu wa Marekani katika vita dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali ya dini ya Kiislamu, imekiri kuwepo matatizo katika upelelezi kuhusu nyendo za Bin Laden na imeamrisha uchunguzi ufanyike, licha ya kwamba inajitahidi kuondowa shaka kuwa Osama huenda ana usaidizi wa aina fulani alioupata kutoka mashirika ya upelelezi nchini humo.

Pakistan yakasirishwa na Marekani

Nyumba inayosemekana alikuwa akiishi Osama bin Laden kabla ya kifo chake

Nyumba inayosemekana alikuwa akiishi Osama bin Laden kabla ya kifo chake

Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Salman Bashir, amesema hizo ni shutuma za uongo na haziwezi kuthibitishwa kwa njia yoyote, na zinaaibisha jitihada za Pakistan na hususan mashirika ya upelelezi nchini humo.

Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, Leon Panetta, amesema Marekani iliificha Pakistan kuhusu uvamizi huo kwa kuhofia kuwa Osama Bin Laden angearifiwa.

Huku utawala wa Rais Obama ukisherehekea kuuawa kwa mtu aliyekuwa akisakwa kupita kiasi, umelazimika kutetea uhalali wa uvamizi huo baada ya kukiri kuwa Osama bin Laden hakuwa amejihami kwa silaha alipopigwa risasi juu ya jicho la kushoto na kuuawa.

Siku ya Jumatano Rais Obama aliamua kutochapishwa picha za mwili wa Bin Laden akitaja hatari za usalama wa taifa, na kuongeza kuwa Marekani haipaswi kujigamba kwa ushindi.

Licha ya mwili wa Bin Laden kutumbukizwa baharini ili kufuta kabisa alama zake ulimwenguni, huenda sasa makaazi yake katika eneo la Abbottabad yakawa eneo la kumkumbuka kiongozi huyo wa Al Qaeda.

Ushahidi uliopatikana katika makaazi yake umefichuwa kuwa kundi la Al Qaeda lilikuwa linafikiria kufanya shambulio kwenye treni katika eneo lisilojulikana nchini Marekani katika kuadhimisha miaka 10 ya mashambulio ya Septemba 11.

Hata hivyo, maafisa wa usalama wa Marekani hawatilii uzito tishio lolote na wameutaja mpango huo kuwa wa matamanio, lakini unaodhihirisha kuwa Bin Laden alikuwa mtu muhimu katika shughuli za kila siku za Al Qaeda zaidi ya ilivyofikiriwa awali.

Mwandishi: Maryam Abdalla/AFPE
Mhariri: Hamidou Oummilkheir

DW inapendekeza

 • Tarehe 06.05.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/11AfY
 • Tarehe 06.05.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/11AfY

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com