1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama atavuna nini Asia?

Admin.WagnerD5 Novemba 2010

Siku mbili tu baada ya chama chake cha Democrat kuangushwa katika uchaguzi wa Baraza la Congress, Rais Barack Obama wa Marekani anapanda ndege kuelekea Asia, kituo chake cha mwanzo kikiwa ni India. Anafuata nini?

https://p.dw.com/p/Pzre
Rais wa Marekani, Barack Obama na Hu Jhin Tao wa China
Rais wa Marekani, Barack Obama na Hu Jhin Tao wa ChinaPicha: picture-alliance/dpa

Kama ilivyo kwa wanasiasa wengine wa nchi za Magharibi, Rais Barack Obama naye ana kila sababu ya kuitembelea India. Kwanza, India imeinuka kuwa taifa la kwanza katika utoaji wa huduma duniani, pili, uchumi wa India uliweza kuhimili mtikisiko wa uchumi ulioukumba ulimwengu na duniani, ambao uliyaacha Marekani imeumizwa vibaya na, tatu, uchumi wa India umekuja juu kutokana na sekta ya teknolojia, ambayo huko nyuma ilionekana ikimilikiwa na ulimwengu wa Magharibi tu peke yake.

Ila bado, Marekani ni miongoni mwa nchi za Magharibi, ambazo zinaziwekea vikwazo baadhi ya bidhaa za India kwa madai ya ukosefu wa ubora katika bidhaa hizo. Matokeo yake ni kuwa nchi hii ya Bara Hindi hulazimika kuingiza bidhaa nyingi zaidi kutoka Marekani kuliko zile inazosafirisha. Lakini, kama anavyosema mkuu wa Godrej Industries, Adi Godrej, hiki ni kikwazo kilichosimama baina ya mataifa haya mawili.

"Kwa mtazamo wa kuimarisha uhusiano wetu, lingelikuwa jambo jema kwa sasa ikiwa Marekani inatupa fursa ya viwango vyote vya teknolojia, kwani jambo hilo litavisadia viwanda vya India kwa kiasi kikubwa.“ Anasema Godrej.

Jambo jengine linaloyakutanisha mataifa haya mawili ni siasa za Afghanistan, kwani vita vinavyoendelea nchini humo vinazorotesha hali ya usalama ya eneo zima. Wapiganaji wa Kiislam wa Afghanistan wana uhusiano wa karibu na hasimu mkubwa wa India na mshirika wa Marekani katika vita dhidi ya ugaidi, Pakistan. Waziri wa zamani wa usalama wa New Delhi, Brajesh Mishra, anatarajia kwamba mbinyo wa Marekani kwa Pakistan unaweza kusaidia usalama wa India.

Msanii wa India akichora picha ya Rais Barack Obama wa Marekani kabla ya ziara ya kiongozi huyo katika nchi hii ya Bara Hindi
Msanii wa India akichora picha ya Rais Barack Obama wa Marekani kabla ya ziara ya kiongozi huyo katika nchi hii ya Bara HindiPicha: AP

"Tuliuambia utawala wa Marekani kwamba oneni huu ugaidi unaotokea Pakistan ndilo tatizo letu kubwa tunalokabiliana nalo. Natarajia kwamba, sasa Marekani itafahamu kwamba Pakistan imekuwa ikicheza mchezo wa ndumilakuwili." Anasema Mishra.

Lakini pia suala ya ushirikiano katika kiwango cha kimataifa, hasa katika Umoja wa Mataifa, ni jambo litakalozungumziwa kwenye ziara hii ya Rais Obama, kama anavyosema mtaalamu wa mambo ya India katika wakfu wa Uchumi na Siasa mjini Berlin, Christian Wagner:

"Bila ya shaka, kuna mambo mengi ambayo watayazungumzia katika ngazi ya kilimwengu kama vile kufanya kazi pamoja katika taasisi za utawala duniani, kuwa pamoja katika masuala ya mazingira, tabia nchi, nishati na hata uhaulishaji wa teknolojia. Kwa hakika, India ina dhima kubwa kama mshirika wa kiuchumi wa Marekani."

Kama ilivyo Ujerumani, India pia imechaguliwa hivi karibuni kuwa mwanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kwa hivyo, si jambo la sadfa kwamba maendeleo yote haya yanazivutia Marekani, Ujerumani na ulimwengu mzima wa Magharibi kuimarisha uhusiano wao na nchi hii ya Bara Hindi inayoinuka kwa kasi kiuchumi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Cem Sey/ZPR

Mhariri: Josephat Charo