1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama ataka kupunguzwa kwa silaha za nyuklia ulimwenguni

Admin.WagnerD26 Machi 2012

Rais wa Marekani Barack Obama amesema nchi yake inaweza kupunguza silaha zake za nyuklia, na kuzitaka Iran na Korea Kaskazini kuachana na mipango yao ya kiatomiki, ama sivyo zikabiliwe na vikwazo zaidi.

https://p.dw.com/p/14SPN
Rais Barack Obama akitoa hotuba yake mjini Seoul
Rais Barack Obama akitoa hotuba yake mjini SeoulPicha: Reuters

Akizungumza mjini Seoul leo, Rais Barack Obama amesema maendeleo makubwa yamekwishapatikana katika juhudi  hizo za kuondoa au kuhakikisha usalama wa zana za kinyuklia, huku akitoa mifano ya nchi kadhaa ambazo tayari zimechukua hatua ya kuondoa mlundikano wa silaha, na kubashiri kuwa nchi nyingine zaidi zitafanya hivyo katika mkutano huu wa siku mbili.

Hata hivyo ameongeza kuwa anafahamu fika kwamba kuna zana za kinyuklia zinazotosha kuundia silaha nyingi, ambazo hazihifadhiwi kwa usalama wa kutosha. Obama amesema pia kuwa kuna makundi ya kigaidi na ya kihalifu ambayo yana ndoto za kumiliki silaha za kinyukilia, na kupata vifaa vya kuundia mabomu, na kuonya kuwa bado ugaidi wa kutumia silaha za kinyuklia ni kitisho kikubwa zaidi kwa dunia.

Nchi 53 zinashiriki katika mkutano huu unaojadili suala la silaha za nyuklia
Nchi 53 zinashiriki katika mkutano huu unaojadili suala la silaha za nyukliaPicha: AP

Uongozi wa kutoa mfano

Rais Barack Obama amewahimiza viongozi na maafisa wa ngazi za juu kutoka nchi 53 zinazoshiriki katika mkutano huo kuendelea na juhudi za kupunguza kitisho cha nyuklia, akiahidi hatua zaidi kutoka Marekani, ikiwa ni pamoja na kuishawishi Urusi kushiriki katika mpango wa kupunguza silaha za nyuklia. Amesema Marekani ina silaha nyingi za nyuklia kuliko mahitaji yake.

''Naamini kwa dhati kwamba tunaweza kuhakikisha usalama wa Marekani na washirika wetu, na kuendelea kuwa na uwezo wa kukabiliana na kitisho chochote, na wakati huo huo tukipunguza kiasi cha silaha za nyuklia tulicho nacho''. Amesema Rais Obama.

Rais wa Marekani ameongeza shinikizo la kidiplomasia kwa Iran na Korea Kaskazini juu ya mipango ya nyuklia ya nchi hizo, ambayo imeghubika mazungumzo ya viongozi wengi licha ya kutokuwepo kwenye agenda ya mkutano.

Maroketi ya Korea Kaskazini yanayosababisha mvutano
Maroketi ya Korea Kaskazini yanayosababisha mvutanoPicha: KRT TV

Makombora ya Korea Kaskazini

Mivutano imekuwa ikizidi kukua kufuatia azma ya Korea Kaskazini kutuma maroketi ya masafa marefu kati kati mwa mwezi ujao wa April. Korea Kusini imetishia kudungua maroketi ya Korea Kaskazini iwapo yatapita katika anga yake. Japan ilitangaza msimamo kama huo wiki iliyopita. Korea Kaskazini inasisitiza kuwa lengo lake ni kuweka angani satellite kwa ajili ya matumizi ya amani.

Rais Obama ameitaka Korea Kaskazini kuachana na mpango wake huo, au ikabiliwe na kutengwa zaidi.

Alisema, ''Kufikia sasa mngekuwa mmekwishang'amua, kuwa uchokozi wenu na kutaka kuunda silaha za nyuklia hakujakidhi usalama mnaoutaka, badala yake kumeuhatarisha zaidi''

Suala la makombora ya Korea Kazkazini limechukua nafasi kubwa katika mkutano baina ya Rais Obama na mwenzake wa China Hu Jintao. Viongozi hao wamekubaliana kuwa mpango huo wa maroketi unatia wasi wasi, na kuafiki kuendelea kulishughulikia kwa pamoja suala hilo.

Rais Obama pia ameionya Iran, akisema muda wa kupata suluhisho la kidiplomasia kwa mradi wake wa kinyuklia, unakwisha haraka.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu