1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama apania kukamilisha jukumu la Marekani nchini Afghanistan

Mohamed Dahman25 Novemba 2009

Ikulu ya Marekani inapanga kutuma wanajeshi zaidi ya 30 elfu wa ziada nchini Afghanistan

https://p.dw.com/p/KgIt
Rais Barack Obama na washauri wake wajadiliana kuhusu hali nchini AfghanistanPicha: AP

Rais Barack Obama ameahidi kukamilisha jukumu lao nchini Afghanistan wakati akiwa ukingoni mwa kutowa uamuzi wake juu ya kupeleka zadi wanajeshi wa Marekani maelfu kwa maelfu nchini Afghanistan kupambana na wanamgambo wa kundi la Taliban ambao hivi karibuni wamekuwa wakiimarisha harakati zao.

Huku kukiwa na repoti kwamba ataamuru kupelekwa kwa wanajeshi wa Marekani 34,000 zaidi kupambana na wapiganaji wa kundi la Taliban na Al- Qaeda, Obama amesema ameazimia kuutokomeza uasi na hiyo kumaliza miezi kadhaa ya tafakuri baada ya mapumziko ya ya Siku ya Shukrani kwa Mungu hapo kesho.

Obama anayeshutumiwa kwa kutapa tapa katika kufikia uamuzi wa hatua hiyo amesema ataliweka wazi suala hilo kwamba wananchi wa Afghanistan hatimae itabidi washughulikie wenyewe usalama wao na atatowa wito kwa washirika wake barani Ulaya na kwengineko kusaidia.

Kufuatia mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa India Manmohan Singh hapo jana Obama alitoa kauli hii :

Baada ya miaka minane ambapo baadhi ya miaka hiyo nadhani hatukuwa aidha na rasilmali au mkakati wa kuikamilisha kazi hiyo kwa hiyo ni nia yangu kuikamilisha kazi hiyo.

Obama ameongeza kusema kwamba watautan'goa na kuuvunja uwezo wao na hatimae kutokomeza na kuangamiza mitandao yao.Amesema utuklivu wa Afghanisntan ni muhimu kwa mchakato huo.

Obama anakabiliwa na umma uliogawika sana kuhusu vita vya Afghanistan na wito wa wenzake wa chama cha Demokratik kuweka ratiba madhubuti ya kuondolewa kwa vikosi vya Maekani miaka minane baada ya vikosi vinayvoongozwa na Marekani kuivamia Afghanistan kufuatia mashambulio ya Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani.

Amesema ana imani kwamba wakati Wamarekani watakaposikia hoja ya busara ya wazi kwa kile wanachokifanya Afghanistan na vipi wanakusudia kufikia malengo yao watawaunga mkono.

Obama pia amesema dunia nzima ina wajibu wa kusaidia harakati zinazoongozwa na Marekani nchini Afghanistan na tangazo lake litafafanuwa majukumu ya washirika wao wa kimataifa.

Baada ya miezi kadhaa ya tafakuri wakishutumiwa na mahasimu wao wa chama cha Republican kwa kutapatapa katika kutoa uamzui wa hatua hiyo Obama amekuwa na kikao cha tisa na cha mwisho na makamanda wakuu na washauri wake wa usalama hapo Jumatatu.

Rais Obama amekuwa akitafakari maombi kutoka kwa kamanda wa vita wa Afghanistan Generali Stanley McChrystal kupeleka wanajehi 40,000 zaidi kujiunga na wanajeshi wa Marekaniu 68,000 ambao tayari wako nchini Afghanistan.

Maafisa wengine wa serikali ya Marekani akiwemo balozi wa Marekani nchini Afghanistan Karl Eikenberry ameonya dhidi ya kuongeza kiwango cha wanajesi hadi hapo serikali ya Afghanistan itakapokomesha rushwa.

Wizara ya Ulinzi wa Marekani imesema hapo Jumanne washirika wao Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi NATO wataongeza vikosi zaidi iwapo Obama ataamuwa kuamrisha kuongezwa kwa wanajeshi wa Marekani.

Washuirika wa NATO ambao mchango wao wa vikosi umefanya wanajeshi wa kigeni walioko Afghanistan kufikia 110,000 wanatazamiwa kuljadili suala hilo la kutuma vikosi zaidi katika mikutano yao ijayo ya kijeshi mapema mwezi wa Desemba.

Kupamba moto upya kwa harakati za wapiganaji wa itikadi kali za Kiislam umeufanya mwaka 2009 kuwa mwaka mbaya kabisa kwa vikosi vya Marekani na washirika wake nchini Afghanistan uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa na kituo cha televisheni cha CNN umeonyesha kwamba karibu nusu ya Wamarekani wanaunga mkono kupelekwa kwa wanajeshi zaidi maelfu kwa melfu wakati asilimia 45 tu wanaunga mkono vita.

Baadhi ya watu wamekuwa wakinon'gona kwamba muda wa Obama kuendelea kubakia madarakani utaamuliwa na uamuzi wake wa kuundeleza mzozo huo kama vile Vita vya Vietnam vilivyochangia kuondoka madarakani kwa Rais Lyndon Johnson.


Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: M.Abdul-Rahman