1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama aanza ziara rasmi Ethiopia

27 Julai 2015

Rais wa Marekani Barack Obama ameanza ziara rasmi ya siku mbili nchini Ethiopia, akiwa Rais wa Kwanza wa Marekani kuzuru Ethiopia taifa la pili barani Afrika, na ndipo yalipo makao makuu ya Umoja wa Afrika.

https://p.dw.com/p/1G58R
Äthiopien Barack Obama Hailemariam Desalegn PK
Picha: Getty Images/AFP/de Souza

Rais Obama akitokea Kenya alikokuwa kwa ziara ya siku tatu na alikoendesha mkutano wa kimtaifa wa wajasiriamali, amewasili katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa jana jioni na kulakiwa na mwenyeji wake waziri mkuu wa Ethiopia Haile Mariam Desalegn

Rais huyo wa Marekani hii leo amekutana kwa mazungumzo na Desalegn kujadili masuala yanayozihusu nchi zao na baadaye watafanya mkutano wa pamoja na wanahabari.

Mjadala wa mzozo wa Sudan Kusini

Baada ya hapo, Obama atafanya mkutano na viongozi wa kanda hiyo kuhusu mzozo wa Sudan Kusini katika juhudi za kuchukua hatua madhubuti dhidi ya viongozi wa Sudan Kusini iwapo watashindwa kuvimaliza vita hivyo ifikapo kati kati ya mwezi ujao. Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar hawatahudhuria mazungumzo hayo.

Ethiopia ambayo ni mshirika muhimu wa Marekani katika kanda hiyo inashutumiwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu kwa ukiukaji wa haki za binadamu na ukandamizaji wa demokrasia.

Hapo Kesho, Obama atakuwa Rais wa kwanza wa Marekani kuhutubia katika umoja wa Afrika wenye nchi wanachama 54. Rais wa Halmashauri ya umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini Zuma ameisifu ziara hiyo aliyoitaja kuwa ya kihistoria na hatua madhubuti kuelekea kutanua na kuboresha uhusiano kati ya Umoja huo na Marekani.

Äthiopiens Pemierminister Hailemariam Desalegn begrüßt US Präsident Barack Obama in Addis Abeba
Rais Obama akiwasili mjini Addis AbabaPicha: Reuters/J. Ernst

Ethiopia kama Kenya, imekuwa katika mstari wa mbele katika vita dhidi ya waasi wa Al Shabab nchini Somalia. Nchi hizo mbili zina majeshi nchini Somalia kama sehemu ya ujumbe wa kijeshi wa Umoja wa Afrika unaoungwa mkono na Marekani. Suala la usalama linatarajiwa kuwa mojawapo ya ajenda kuu ya mazungumzo kati ya Obama na mwenyeji wake.

Ziara ya Obama nchini Ethiopia inakuja miezi miwili baada ya chaguzi nchini humo ambazo chama tawala kinachoongozwa na Haile Mariam Desalegn kilishinda viti vyote 546 vya bunge.

Vyama vya upinzani vimelalamika kukandamizwa na serikali na kudai serikali ilitumia mbinu za kiimla kushinda katika uchaguzi huo.

Obama kuzungumzia masuala ya demokrasia

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema inatambua kuwepo vizuizi vya uhuru wa kujieleza, kuwepo kesi zinazochochewa kisiasa na kuteswa na kukandamizwa kwa wanasiasa wa upinzani na wanahabari Ethiopia.

Masuala hayo ya demokrasia yanatarajiwa kuangaziwa katika ziara hiyo ya kiongozi wa Marekani nchini Ethiopia ikizingatiwa alizungumzia wazi masuala ya haki za binadamu na ufisadi nchini Kenya mwishoni mwa juma. Obama pia atafanya mazungumzo na viongozi wa mashirika ya kiraia.

Licha ya rekodi mbaya ya haki za binadamu na kutokuwepo kwa uhuru wa kidemokrasia, Ethiopia imepiga hatua za kipigiwa mfano kutoka kuwa taifa maskini lililojulikana duniani kwa baa la njaa lililoikumba mwaka 1984 na kukua kiuchumi, kuimarika pakubwa katika miundo mbinu na kuwa mojawapo ya nchi za Afrika zinazovutia wawekezaji. Marekani inatafuta kuimarisha uhusiano wa kibiashara na taifa hilo.

Mwandishi:Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Gakuba Daniel