1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama aidhinisha mashambulizi ya angani Iraq

8 Agosti 2014

Rais wa Marekani Barack Obama ameziagiza ndege za kivita kurudi tena Iraq kudondosha chakula kwa wakimbizi na ikihitajika zifanye mashambulizi kuzuwia kile alichokiita uwezekano wa mauaji ya halaiki.

https://p.dw.com/p/1CrEx
USA Präsident Barack Obama in Washington zu Lage in Irak Kurden IS
Picha: Reuters

Jukumu la kwanza la operesheni hiyo lilikuwa kuwadondoshea chakula maelfu ya waumini wa kundi la wachache la madhehebu ya Yazidi waliozingirwa na wapiganaji wa kisunni kwenye mlima Sinjar.

Obama alisema kwamba alikuwa ameliruhusu jeshi kufanya mashambulizi ya makhsusi kwa lengo la kuvisaidia vikosi vya Iraq kuwazuwia wapiganaji wa Kisunni kusonga mbele, au kuwalinda washauri wa kijeshi wa Marekani wanaofanyakazi nchini humo.

Rais huyo alisema ndege za kijeshin zinaweza kuwalenga wapiganaji wa Dola ya Kiislamu ikiwa watajaribu kusonga mbele kuelekea mji wa Arbil, ambako Marakeni ina uwepo wa kidiplomasia na washauri wa jeshi la Iraq.

Wakristu na waumini wa Yazidi wa Iraq wakikimbia mapigano.
Wakristu na waumini wa Yazidi wa Iraq wakikimbia mapigano.Picha: picture alliance/AA

"Kwa maombi ya serikali ya Iraq, tumeanza operesheni ya kuwasaidia raia waliokwama kwenye mlima. Maelfu ya Wairaq wamepoteza makaazi, na ripoti zinazotoka huko zinawaelezea wapiganaji wa IS wakizizingira familia, kufanya mauaji ya makundi na kuwageuza wanawake wa Yazidi kuwa watumwa," alisema Obama.

Kitisho cha kuangamizwa

Afisa mwandamizi wa wizara ya ulinzi alithibitisha kuwa ndege za Marekani tayari zimedondosha chakula na maji kwa maelfu ya raia wa Iraq, akimaanisha Wayazidi waliokwama kwenye mlima Sinjar kaskazini mwa Iraq. Obama alikiri kuwa Marekani haiwezi kuchukuwa hatua kila mara haki inapovunjwa, lakini alisisitiza kuwa wanaweza kuchukuwa hatua kwa uzingativu ili kuepusha uwezekano wa kutokea mauaji ya halaiki.

"Tunapokabiliwa na hali kama tulio nayo kwenye mlima huo, ambako watu wasio na hatia wanakabiliwa na kitisho cha kuangamizwa kwa kiwango kikubwa, tukiwa na idhini ya kusaidia, katika hali hii maombi kutoka kwa serikali ya Iraq, na tunapokuwa na uwezo wa kipekee wa kusaidia kuepusha mauaji, naamini Marekani haiwezi kukaa na kufumba macho."

Mapema mjini New York, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa liliitaka jamii ya kimataifa kuisadia serikali ya Iraq na watu wake, na kufanya kila inaloweza kuwaondolea mateso raia. Ofisi ya rais wa Ufaransa Francois Hollande, ilisema kuwa Ufaransa ilikuwa tayari kuvisaidia vikosi vinavyoshiriki katika vita hivyo.

Obama aliingia madarakani na dhamira ya kukomesha ushiriki wa kijeshi wa Marekani nchini Iraq, na katika muhula wake wa kwanza aliondoa idadi kubwa ya wanajeshi wa ardhini waliopelekwa huko tangu uvamizi wa Marekani mwaka 2003.

Wapiganaji wa kundi la Dola ya Kiislamu wakiwa mazoezini.
Wapiganaji wa kundi la Dola ya Kiislamu wakiwa mazoezini.Picha: picture-alliance/abaca

IS wajivunia ushindi

Lakini mafanikio ya hivi karibuni ya kundi la Dola ya Kiislamu, yalimlazimu kuwatuma tena washauri wa kijeshi mjini Baghdad ili kutathmini hali inayozidi kudorora. Wasunni wa Iraq wanapambana na serikali ya waziri mkuu Nouri al-Maliki wanayemtuhumu kwa kuwakandamiza na kuwatenga katika uteuzi wa nafasi za serikalini.

Mwishoni mwa mwezi Juni IS ilitangaza kuundwa kwa dola ya Kiislamu kuanzia kwenye maeno yanayodhibitiwa na waasi nchini Syria na Iraq na iliuteka mji wa muhimu wa Mosul, na imekuwa ikichukuwa maeneo zaidi kila kukicha. Kundi hilo limejivunia ushindi wake wa karibuni kwa kutangaza kile lilichokiita "ukombozi mwingine wa maeneo ya mkoa wa Nineveh, na kuwapa somo Wakurdi wasiyoegemea dini."

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe.

Mhariri: Josephat Nyiro Charo.