1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nusu ya Warepublican watakataa ushindi wa Clinton

Caro Robi
22 Oktoba 2016

Uchunguzi mpya wa maoni nchini Marekani umeonyesha kuwa asilimia hamsini ya Warepublican nchini humo hawatakubali ushindi wa mgombea urais wa chama cha Democratic Hillary Clinton.

https://p.dw.com/p/2RY3S
USA | 3. Präsidentschaftsdebatte 2016 in Las Vegas
Picha: picture-alliance/AP Photo/Patrick Semansky

Asilimia 70 ya wapiga kura wa Democrats wamesema watakubali ushindi wa mgombea urais wa Republican Donald Trump. Uchunguzi huo wa maoni uliotolewa jana Ijumma na shirika la habari la Reuters na shirika linaloendesha uchunguzi wa maoni la Ipsos ni kufuatia madai ya mara kwa mara ya Trump kuwa vyombo vya habari na mfumo wa uchaguzi nchini Marekani vina njama ya kufanya udanganyifu wa kura ili kumwangusha.

Trump amesema atakubali matokeo ya uchaguzi iwapo tu ataibuka mshindi. Mgombea huyo wa urais amewataka wafusai wake kuwa chonjo siku ya uchaguzi kuzuia wapiga kura wasiostahili kupiga kura.

Kwa upande wake Bi Clinton amesema atakubali matokeo jinsi yatakavyokuwa. Serikali ya Marekani imeishutumu Urusi kwa kuendesha kampeini ya udukuzi wa mitandao na mawasiliano dhidi ya chama cha Democratic na mfumo wa uchaguzi Marekani.

Kura hiyo ya maoni inaonyesha kuna wasiwasi katika ulingo wa siasa kuhusu masuala ya uchaguzi kama wapiga kura bandia, kurubuniwa kwa wapiga kura na kuhusu jinsi kura zitakavyohesabiwa.

Warepublican saba kati ya kumi wana wasiwasi kuhusu kununuliwa kwa kura, kuwepo mashini zenye hitilafu za kupigia kura au kuwepo uchakachuaji mwingine wakati wa uchaguzi. Wademocrat sita kati ya kumi ndiyo wanahisi hayo yatakuwa matatizo wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa tarehe 8 Novemba.

US TV Debatte Trump vs Clinton
Wagombea urais wa Marekani Donald Trump na Hillary ClintonPicha: Getty Images/C. Somodevilla

Kura za maoni bado zinamuweka Bi Clinton mbele ya mpinzani wake Trump ambaye ameshutumiwa vikali kuhusiana na kauli chafu na misimamo yake mikali kuwahusu wanawake, waislamu, wageni, vyombo vya habari na kutokuwa na tajriba ya kisiasa na uongozi.

Vigogo kadhaa wa chama chake cha Republican akiwemo kiongozi wa chama hicho Spika wa bunge la Marekani Paul Ryan pia wametangaza hadharani hawatamuunga mkono Trump.

Kulingana na kura za maoni za hivi punde Bi Clinton, waziri wa zamani wa mambo ya nje na mke wa Rais wa zamani wa Marekani anaongoza kwa asilimia 44 dhidi ya Trump mfanyabiashara tajiri aliye na asilimia 40. Mapema mwezi huu Clinton alikuwa akiongoza kwa asilimia 44 dhidi ya Trump aliyekuwa na asilimia 37.

Bi Clinton amesema mpinzani wake ni kitisho kwa demokrasia ya Marekani baada ya kukataa kuahidi kuheshimu na kukubali matokeo ya uchaguzi na kuongeza kuna tofauti kati ya uongozi na udikteta na mojawapo ya mambo ya kutofautisha hilo, ni kukabidhi madaraka kwa njia ya amani.

Clinton ambaye anaazimia kuwa mwanamke wa kwanza kuiongoza Marekani amefanya kampeini kabambe katika jimbo la Ohio. Anaongoza kwa idadi ndogo katika jimbo la North Carolina na Arizona, ila ana uungwaji mkono mkubwa katika majimbo ya Florida, Pennsylvania na Virginia.

Trump alifanya kampeini katika jimbo la Pennsylvania na Ohio ambako anatarajiwa kukita kambi tena leo akizingatia hakuna mgombea wa Republican ashawahi kushinda katika jimbo la Ohio.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/afp

Mhariri: Bruce Amani