1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vurugu zatawala uchaguzi Burundi

21 Julai 2015

Raia wa Burundi wanapiga kura Jumanne hii katika zoezi lililoghubikwa na milio ya risasi na miripuko ya magruneti, huku rais Pierre Nkurunziza akitazamiwa kushinda muhula wa tatu licha ya ukosoaji wa kimataifa.

https://p.dw.com/p/1G20Z
Afrika Wahl in Burundi Proteste
Picha: Getty Images/AFP/C. De Souza

Tayari watu wasiopungua wawili wameuawa -- akiwemo askari moja wa polisi na raia katika mkururu wa miripuko na mashambulizi ya risasi usiku wa kuamkia Jumanne, polisi na mashuhuda wamesema.

Mripiko na ufyetuaji risasi vilisikika pia wakati vituo vya kupigia kura vikianza kufunguliwa alfajiri katika mji mkuu Bujumbura, ambao ndiyo kitovu cha maadamano ya kupinga azma ya Nkurunziza kuwania muhula wa tatu.

Wapinzani wanamtuhumu Nkurunziza kwa kukiuka katiba kwa hatua yake ya kuwania muhula mwingine wa miaka mitano madarakani.

Wafadhali wa magharibi na mataifa ya Kiafrika yalio na mashaka kuhusu wasiwasi katika kanda hiyo yenye historia ya migogoro ya kikabila, waliitaka Burundi iahirishe uchaguzi huo. Lakini serikali inasema tayari imeshaahirisha uchaguzi huo vya kutosha na iliahidi kura ya haki.

Mwili wa mwanaume alieuawa usiku wa kuamkia Jumanne ukiwa umefunikwa barabarani waakati vituo vya kupigia kura vikifunguliwa.
Mwili wa mwanaume alieuawa usiku wa kuamkia Jumanne ukiwa umefunikwa barabarani waakati vituo vya kupigia kura vikifunguliwa.Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

Hali ya kupooza katika baadhi ya vituo

Karibu watu milioni 3.8 wana haki ya kupiga kura. Wakati zoezi hilo likiendelelea, mwandishi wa DW mjini Bujumbura amesema hali ya ukimya katika baadhi ya vituo vy akupigia kura mjini humo, kukiwa na watu foreni chache na fupi.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametoa wito wa kuwepo na utulivu, na kuzitaka pande zote kujiepusha na vuitendo vya vurugu vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa Burundi na kanda nzima. Wakosoaji wanahofu kuwa ushindi wa rais Nkurunziza utakuwa wa hila na kumuacha aendelee kuitawala nchi iliyogawanyika vibaya.

Katika kituo kimoja, cha shule ya Saint-Etienne kilichopo katikati mwa mji mkuu, wapigakura wameonekana wakipangusa wino kwenye vidole vyao ili kuepuka kulipizwa kisasi na wafuasi wa upinzani waliosusia uchaguzi. "Sitakim kurudi nyumbani nikiwa na wino kwenye vidole vyangu," alisema mpigakura moja.

Huku uchaguzi huo ukiwa umepingwa na upinzani kama kichekesho, Nkurunziza mwenye umri wa miaka 51 -- muasi wa zamani, muumini wa kilokole na shabiki mkubwa wa kandandanda, hakabiliwi na ushindani wowote wa maana.

"Licha ya kuwepo na vyama vingi vya siasa, huu ni uchaguzi wa mgombea mmoja tu, ambako Warundi tayari wanajua matokeo," amesema Thierry Vircoulon kutoka kundi la kimataifa la kushughulikia migogoro ICG, ambalo limeonya kuwa hali nchi humo ina kila dalili za kuanzisha vita vipya vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwanamke akipatiwa karatasi za kura katika kituo kilichopa mjini Bujumbura.
Mwanamke akipatiwa karatasi za kura katika kituo kilichopa mjini Bujumbura.Picha: Reuters/M. Hutchings

Ukandimizaji dhidi ya wapinzani

Maandamano ya kumpinga Nkurunziza yamekandamizwa vibaya na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 100 tangu mwishoni mwa mwezi April. Vyombo huru vya habari vimefungwa na wapinzani wengi wamekimbia -- na kuungana na Warundi zaidi ya 150,000 wa kawaida wanaohofu kuwa nchi yao huenda ikakumbwa na vurugu mpya.

Shirika la misaada la Madaktari wasio na mipaka MSF lilisema siku ya Jumatatu kuwa karibu watu 1000 walikuwa wanakimbilia nchini Tanzania kila siku, "kwa kuvuka mpaka kupitia msitu.. na wengi wao wakisafiri kwa miguu gizani na bila bila kubeba kitu chochote."

Katikati mwa mwezi Mei majenerali waasi walijaribu kumpindua Nkurunziza lakini baada ya kushindwa katika jaribio hilo walianzisha uasi kaskazini mwa nchi. Mazungumzo ya dakika za mwisho yaliyoongozwa na Uganda kujaribu kutatua mgogoro huo yalivunjika siku ya Jumapili. "Wamekataa kuinusuru Burundi kutokana na machafuko," alisema kiongozi wa upinzani Jean Miani, ambaye alisusia uchaguzi huo kama wengine.

Kiongozi mkuu wa upinzani Agathon Rwasa, hajajiondoa rasmi, lakini alisema uchaguzi huo hauwezi kuwa huru na wa haki na wala hakuendesha kampeni yoyote. Wachambuzi wanasema mgogoro mpya nchini humo unaweza kuwasha upya vurugu za kikabila kati ya Wahutu na Watutsi na kusababisha janga jengine la kibinaadamu katika kanda hiyo.

Mgogoro huo pia unatishia kuzivuta nchi jirani -- kama ilivyotokea katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Vita vya mwisho vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi vilisababisha vifo vya watu wasiopungua 300,000.

Rais Pierre Nkurunziza anatarajiwa kushinda kwa kishindo baada ya wapinzani kususia uchaguzi.
Rais Pierre Nkurunziza anatarajiwa kushinda kwa kishindo baada ya wapinzani kususia uchaguzi.Picha: picture-alliance/dpa/C. Karaba

Mambo ni yale yale

Chama cha Nkurunziza cha CNDD-FDD kilipata ushindi mkubwa uliyotaraajiwa katika uchaguzi wa bunge uliyofanyika Mei 29 ambao pia ulisusiwa na upinzani. Waangalizi wa Umoja wa Mataifa -- ambao ndiyo chombo pekee cha uangalizi cha kimataifa katika uchaguzi wa Jumanne -- ulisema duru ya mwisho ya uchaguzi ilifanyika katika "mazingira ya hofu na vitisho."

Uchaguzi wa bunge ulichukuwa wiki nzima kutangazwa. Uchaguzi wa rais unatazamiwa kuchukuwa muda kama huo, wamesema wanadiplomasia, hii ikimaanisha kuwa Nkurunziza -- ambaye taifa lake linategemea zaidi msaada -- yumkini akakabiliwa na kutengwa kimataifa.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre.

Mhariri: Mohammed Khelef.