1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nkurunziza afanya mabadiliko ya mawaziri

Amida ISSA20 Aprili 2018

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza amelifanyia marekebisho Baraza lake la mawaziri. Katika jumla ya mawaziri 21 wanaounda serikali hiyo, wapya ni wanne huku wengine wakisalia kwenye nyadhifa zao

https://p.dw.com/p/2wO0V
Burundi Präsident Nkurunziza arrives for the celebrations to mark Burundi's 55th anniversary of the independence at the Prince Louis Rwagasore stadium in Bujumbura
Picha: Reuters/E. Ngendakumana

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza amelifanyia marekebisho Baraza lake la mawaziri, ambapo miongoni mwa walioondolewa ni waziri wa mambo ya kigeni, Allain Aime Nyamitwe, baada ya kuzungumziwa uhusiano usio mzuri kati yao kufuatia sheria mpya inayopiga marufuku kugombea urais na kukalia nyadhifa muhimu serikali urais watu wenye uraia wa nchi mbili. Waziri mpya wa mambo ya nje, Ezekiel Ninbigira, ni mkuu wa zamani wa tawi la vijana wafuasi wa chama tawala, mashuhuri kama Imbonerakure, ambalo taarifa za mashirika kadhaa ya kimataifa zinalihusisha na machafuko na mauaji katika taifa hilo la Afrika ya Kati.

Katika jumla ya mawaziri 21 wanaounda serikali hiyo, wapya ni wanne huku wengine wakisalia kwenye nyadhifa zao.

Miongoni mwa walioaga serikali ni pamoja na Allain Aime Nyamitwe, aliyekuwa waziri wa mambo ya kigeni. Wizara hiyo imekabidhiwa kwa Ezekiel Niragira, balozi wa Burundi nchini Kenya, na mkuu wa zamani wa tawi la vijana la chama cha CNDD-FDD liitwalo Imbonerakure.

Waziri Nyamitwe ameondolewa serikalini baada ya kuzungumzia uhusiano uliofifia kati ya ndugu wawili, Willy Nyamitwe ambaye ni mshauri wa rais na yeye Alain na Rais Nkurunziza. Ndugu hao wanatajwa kutoridhishwa na sheria iliyosainiwa na Rais Nkurunziza ambayo inampiga marufuku kugombea urais na hata kushika nyadhifa nyingine muhimu serikalini mtu mwenye uraia wa nchi mbili. Ndugu hao wawili wana uraia wa nchi mbili.

Alain Nyamitwe aliyekuwa waziri wa mambo ya nchi za nje ni miongoni mwa waliotimulia serikalini
Alain Nyamitwe aliyekuwa waziri wa mambo ya nchi za nje ni miongoni mwa waliotimulia serikaliniPicha: DW/F.K. Tiassou

Sheria hiyo ilitajwa kama haikuwaridhisha akina Nyamitwe, ambao wamekuwa waungaji mkono wakubwa wa Rais Nkurunziza kwa muda wote wa mzozo huu uliozuka Burundi mwaka 2015.

Rais hajatoa maelezo ya kufanya marekebisho hayo

Wengine waloiaga serikali ni pamoja na waziri wa afya Josiane Nijimbere na yule wa utangazaji habari, Nestor Bankumukunzi.

Wapya katika serikali hiyo wametajwa kutokuwa na umaarufu katika uwanja wa siasa nchini. Nyadhifa nyingine kama mambo ya ndani, sheria na usalama zimesalia na mawaziri wake. Hata hivyo, hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa na msemaji wa rais juu ya sababu zilizopelekea serikali kurekebishwa.

Marekebisho hayo katika serikali yamekuja pasi na kuwepo uvumi wowote kwenye vyombo vya habari nchini Burundi, wakati hali ya usalama ikionekana kuzidi kutia hofu. Bado mauwaji yanaripotiwa kuendelea kushuhudiwa. Kiijana Rodrigue Nzeyimana, mtoto wa mwanasiasa wa zamani maarufu wa upinzani, alitoweka tangu mwishoni mwa wiki.

Vile vile mabadiliko haya ya baraza la mawaziri yanakuja zikisalia siku chache kabla ya kufanyika kura ya maoni juu ya marekebisho ya katiba, ambayo upinzani umeitaka jamii ya kimataifa kufanya kila liwezekanalo ili kusimamisha mchakato huo ilioutaja kuwa kuirudisha Burundi katika matatizo.

Mwandishi: Amida ISSA/DW Bujumbura
Mhariri: Mohammed Khelef