1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Njama ya mapinduzi Mali

1 Mei 2012

Viongozi wa utawala wa kijeshi wa Mali wamesema "wanaidhibiti hali ya mambo" baada ya mapigano dhidi ya vikosi tiifu kwa rais wa zamani, Amadou Toumani Touré. Watu kadhaa wameuwawa.

https://p.dw.com/p/14nVo
Mkuu wa utawala wa kijeshi nchini Mali Amadou SanogoPicha: Reuters

Alfajiri ya leo, mwakilishi wa utawala wa kijeshi ulioingia madarakani baada ya kupinduliwa rais Amani Toure Machi 22 iliyopita, alionekana katika televisheni akiwatuliza wananchi, huku akisema "hali ni salama mjini Bamako baada ya "mashambulio anayosema yamelengwa kuvuruga utaratibu wa kurejesha nidhamu na kuheshimu katiba.

Watu wasiojulikana na wenye dhamiri mbaya wameishambulia kambi ya kijeshi ya Kati, kituo cha Radio na Televisheni ya taifa na kiwanja cha ndege cha kimataifa mjini Bamako.Vituo vyote hivyo hivi sasa vimekombolewa na vinadhibitiwa na vikosi vya jeshi na vya usalama."Amesema.

Mwanajeshi huyo ambae hajulikani ni nani, anasema waasi hao wamesaidiwa na watu kutoka nje. Mwanajeshi huyo amesema waasi kadhaa wamekamatwa na kuahidi wote wale wanaohusika watasakwa na kufikishwa mahakamani.

Mali Putsch Übergangspräsident Dioncounda Traore
Rais wa kipindi cha mpito Dioncounda TraorePicha: picture-alliance/dpa

Muda mfupi kabla ya tangazo hilo la televisheni, mkuu wa utawala wa kijeshi, kepteni Amadou Haya Sanogo, alisema pia kwa njia ya televisheni, kwamba "wanaidhibiti hali ya mambo mjini Bamako," ambayo mashahidi wanasema inatatanisha.

Duru za kuaminika na mashahidi walisema hapo awali kituo cha Radio na Televisheni ORTM na uwanja wa ndege wa kimataifa vinadhibitiwa na kikosi cha rais-mashuhuri kwa jina la "vikofia vyekundu"-wanaomtii rais wa zamani Amadou Toumani Touré.

Kituo cha kibinafsi cha Radio Kayira mara kadhaa kilikuwa kikitangaza taarifa inayosemekana ni ya kepteni Sanogo inayolaani kuwepo kwa mamluki na wanajeshi wa kigeni wanaowasaidia wanajeshi wa rais wa zamani.

Shahidi mmoja anasema:"Kuna majeshi yaliyoingia katika kituo cha Radio na Televisheni, yakaanza kufyetua risasi ovyo ovyo na kusababisha vurugu na mtafaruku."

Njia inayounganisha mji mkuu Bamako na kambi ya kijeshi ya Kati, makao makuu ya viongozi wa kijeshi, imefungwa na wanajeshi walio watiifu kwa rais wa zamani, ATT-hayo ni kwa mujibu wa duru za kibalozi.

Mashahidi wanasema mapigano yalianza mjini Bamako pale vikosi vilivyo tiifu kwa ATT vilipopinga kukamatwa mkuu wa zamani wa vikosi vya wanajeshi, Abidine Guindo, na askari kanzu wa utawala wa kijeshi.

Abidjan ECOWAS Treffen Macky Sall Alpha Conde Faure Gnassingbe
Mkutano wa viongozi wa ECOWAS mjini AbidjanPicha: Reuters

Machafuko haya yanasadifu muda mfupi baada ya kuakhirishwa mkutano uliopangwa kufanyika Ouagadougou kati ya wawakilishi wa utawala wa kijeshi na rais wa Bourkina Fasso-Blaise Compaore, mpatanishi wa mgogoro wa Mali, baada ya kepteni Sanogo kuubadilisha msimamo wake na kukataa kutumwa wanajeshi wa ECOWAS pamoja pia na kipindi cha mpito cha miezi 12, kama ilivyoshauriwa na viongozi wa jumuia ya uchumi ya Afrika Magharibi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir:AFPZReuters

Mhariri: Miraji Othman