1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria yatinga 16 bora licha ya kipigo

26 Juni 2014

Nigeria ilifanikiwa kusonga mbele katika raundi ya 16 licha ya kushindwa na Argentina kwa magoli 3-2, shukrani kwa ushindi wa Bosnia wa magoli 3-1 dhidi ya Iran.

https://p.dw.com/p/1CQFV
Fußball WM 2014 Argentinien Nigeria Tor
Picha: Reuters

Wakati masuali yanaendelea kuhusu uwezo wa Argentina kama mmoja ya timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa kombe hilo, mchezo uliyoonyeshwa na nyota wao Lionel Messi katika awamu hii ya makundi umewakuna mashabiki, wachezaji wenzake, makocha na hata wapinzani.

Kocha wa Nigeria Stephen Keshi, alimsifu nyota huyo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya mechi ya jana, akimfananisha na mchezaji alietoka katika sayari ya Jupita. Nigeria waliingia mchuano huo wakiwa timu pekee ambayo ilikuwa haijafungwa bao, lakini walikuwa hawajakumbana na timu yenye ubora wa Argentina, ambao waliitia kishindo.

Ufaransa ilitoka sare ya bila kufungana na Ecuador.
Ufaransa ilitoka sare ya bila kufungana na Ecuador.Picha: Reuters

Wakijifaharisha kwa mfumo wao wa mashambulizi unaoundwa na kina Messi, Sergio Aguero, Gonzalo Higuain na Angel Di Maria, Argentina walikuwa wameweza kufunga magoli matatu tu katika mechi mbili. Lakini nyota hao wanne walionyesha mchezo bora dhidi ya Nigeria, huku safu yao ya mashambulizi ikiongozwa na Messi, ambaye alifunga mara mbili katika kipindi cha kwanza, na alionekana wa hatari muda wote wa mchezo.

Ecuador nje, Ufaransa, Uswisi zafuzu

Ufaransa na Ecuador zilitoka sare ya bila kufungana katika mchezo wao wa mwisho wa kundi E, sare ambayo imewapeleka Ufaransa katika raundi ya pili wakiwa vinara wa kundi hilo, na kuwaondoa wapinzani wao kutokana na ushindi wa Uswisi wa magoli 3-0 dhidi ya Honduras.

Mlinda mlango wa Ecuador Alexander Dominguez aliokoa mikwaju miwili na kuwanyima magoli Paul Pogba na Antoine Griezmann, lakini timu hiyo ya Amerika Kusini ilipata pigo dakika tano baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, baada ya nahodha wao Antonio Valencia kutolewa nje kwa kosa la kumshika Lucan Digne wakati wawili hao wakigombania mpira.

Ufaransa inaongoza kundi hilo kwa pointi saba na itacheza dhidi ya washindi wa pili wa kundi F Nigeria, wakati Uswisi, ambao wamemaliza wakiwa na pointi sita, watakabiliana na washindi wa kundi F Argentina. Ecuador wamemaliza wakiwa na pointi nne, na kuwa timu pekee kati ya sita za Amerika Kusini kutofuzu, wakati Honduras walipoteza michezo yao yote mitatu.

Xherdan Shaqiri akishangilia baada ya kuifunga Honduras
Xherdan Shaqiri akishangilia baada ya kuifunga HondurasPicha: Reuters

"Hat-trick" ya pili ya mashindano

Xerdan Shaqiri alifunga Hat-trick - yaani magoli matatu, wakati Uswisi ikiichapa Honduras magoli 3-0 mjini Manaus. Waswisi walianza kuongoza katika dakika ya sita wakati Shaqiri alipomzuwia beki wa kushoto Juan Carlos Garcia na kuachia mkwaju kutoka nje ya box, ambao ulimpita mlinda mlango Noel Valladares.

Aliongeza goli la pili katika dakika ya 31 kufuatia pasi ya Josip Drmic na wawili hao walishirikiana tena katika dakika ya 71 wakati Shaqiri alipokamilisha hat-trick yake. Hiyo ilikuwa hat-trick ya pili ya kombe la dunia 2014, baada ya magoli matatu ya Thomas Müller aliyoifungia Ujerumani dhidi ya Ureno, na ya 50 katika historia ya mashindano ya kombe la dunia.

Leo jioni wawakilishi wengine wa Afrika Ghana watakuwa dimbani dhidi ya Ureno katika kundi G. Ujerumani itamenyana na Marekani, huku Korea Kusini ikiumana na Ubelgiji na Algeria ikitupa karata yake dhidi ya Urusi katika michezo ya mwisho ya kundi H.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ape,dpae,rtre.
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman