1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria yaomba dawa ya majaribio ya Ebola

Admin.WagnerD13 Agosti 2014

Nigeria imeomba kupatiwa dawa ya majaribio ya Ebola ya ZMapp Jumatano, wakati ambapo nchi hiyo ikiripoti kifo cha tatu kutokana na virusi hivyo vinavyozidi kuichachafya kanda ya Afrika Magharibi.

https://p.dw.com/p/1CtMu
Ebola in Westafrika
Picha: Reuters

Waziri wa mawasiliano wa Nigeria Labaran Maku alisema serikali ya nchi hiyo imetuma maombi kwa kituo cha kuzuwia magonjwa nchini Marekani CDC kupatiwa dawa hiyo ambayo haijathibitishwa ili kuwatibu watu walioathirika, na kwamba walikuwa wanasubiri majibu kutoka Washington.

Maombi hayo yamekuja siku moja baada ya shirika la afya duniani WHO, kusema kuwa wagonjwa wanaweza kupatiwa dawa ambazo hazijathibitishwa kwa kuzingatia ukali wa mripuko wa Ebola, ambao ndiyo mbaya zaidi katika historia.

Wafanyakazi wa shirika la misaada la MSF wakiwandalia chakula wagonjwa wa Ebola katika kambi ya Kailahun nchini Sierra Leon.
Wafanyakazi wa shirika la misaada la MSF wakiwandalia chakula wagonjwa wa Ebola katika kambi ya Kailahun nchini Sierra Leon.Picha: Reuters

Canada yajibu wito

Wakala wa afya ya jamii nchini Canada, ulisema unaweza kutuma kati ya dozi 800 na 1,000 za dawa tofauti za majaribio kwa WHO. Dozi kumi za dawa iitwayo VSV-EBOV tayari zimetumwa katika hospitali mjini Geneva, kwa maombi ya WHO, na kwa shirika la misaada la Madaktari wasio na Mipaka MSF.

Nigeria ndiyo nchi ya pili kuomba dawa ya ZMapp. Liberia iliomba dozi za dawa hiyo, ambayo imeripotiwa kutumiwa kwa madaktari wawili nchini humo. ZMapp pia ilitumiwa kwa wafanyakazi wawili wa misaada wa Marekani, ambao wanasemekana kuonyesha nafuu, na Mmishonari wa Uhispania, aliefariki jana Jumanne mjini Madrid.

Maombi mashakani

Lakini haikubainika mara moja iwapo maombi ya Nigeria yatajibiwa, kwa sababu kampuni ya Marekani inyotengeneza dawa ya ZMapp ilisema katika tarifa kuwa ilikuwa imemaliza dawa ndogo iliyokuwa nayo. Kifo kipya kilichoripotiwa nchini Nigeria leo kinafanya jumla ya watu waliofariki kutokana na ugonjwa huo nchini humo kuwa watatu

Afisa wa serikali Jatto Asihu Abdulqadir, mwenye umri wa miaka 36 alikuwa na mawasiliano na mshauri wa serikali ya Liberia Patrick Sawyer, ambaye alikuwa mtu wa kwanza kufariki kwa ugonjwa wa Ebola nchini Nigeria Julai 25. Watu kumi wamethibitishwa kuwa na ugonjwa huo nchini Nigeria, na 139 wanachunguzwa kwa mujibu wa wizara ya afya ya nchi hiyo.

Mbadilishaji wa fedha wa Liberia akiosha mikono yake baada ya kuwahudumiwa wateja kama moja ya njia za kujihadhari.
Mbadilishaji wa fedha wa Liberia akiosha mikono yake baada ya kuwahudumiwa wateja kama moja ya njia za kujihadhari.Picha: picture-alliance/dpa

Gambia, Cote di'Voire na Zambia zilipiga marufuku safari za ndege kutoka Nigeria, na wasafiri wa Zambia na Nigeria watawekwa katika karantini kwa muda wa siku 30 kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini. Kuna kesi 1,800 za maambukizi ya ugonjwa huo zilizothibitishwa na vifo zaidi ya 1000 kufikia Agosti 9, lilisema shirika la WHO.

Sekta ya michezo yaguswa pia

Wakati huo huo, Ebola imezusha hofu katika sekta ya michezo ya Afrika, baada ya Shelisheli kuwakatilia wachezaji wa Sierra Leon kuingia nchini humo kwa ajili ya mechi ya kufuzu mashindano ya kombe la Afrika, na nchi hiyo kujitoa kabisaa katika mechi za kufuzu mashindano hayo.

Sierra Leon na Liberia, mbili kati ya nchi nne ambako kandanda inapendwa zaidi Afrika Magharibi, zimesitisha michezo yote ya kandanda katika mataifa yake. Maafisa wa afya wanasema kuna hatari kubwa iwapo watu wataruhusiwa kukusanyika katika makundi makubwa.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ape,dpae/rtre
Mhariri: Josephat Nyiro Charo