1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria yafufua matumaini yake kombe la dunia

Sekione Kitojo
23 Juni 2018

Nigeria ilifufua matumaini yake katika kombe la dunia nchini Urusi jana Ijumaa (22.06.2018)kwa kuilaza Iceland kwa mabao 2-0, kwa  mabao yaliyofungwa na mshambuliaji Ahmed Musa

https://p.dw.com/p/307k5
Russland WM 2018 l Nigeria vs Island – Tor 1:0  Ahmed Musa
Picha: Reuters/T. Hanai

Kipigo ilichopata Iceland dhidi ya Nigeria, Iceland ikiwa  imefika  kwa  mara  ya  kwanza katika  fainali  za  kombe  la  dunia, hakikuzika ndoto  yao  bado, wakati  Argentina inayoyumba  yumba  inaweza  pia  kujinasua katika  dakika  za  mwisho na  kuingia  katika  awamu  ya  mtoano.

Russland WM 2018 l Nigeria vs Island – Tor 1:0  Ahmed Musa
bao la kwanza la Ahmed Musa wa nigeria dhidi ya IcelandPicha: Getty Images/K. C. Cox

Lakini  ushindi  wa  jana Ijumaa, kusini  mwa  Urusi, unashuhudia Nigeria  ikiwa  katika  udhibiti  wa  majaaliwa  yake wakati watakapokutana  na  Argentina katika  mchezo  wao  wa  mwisho wa kundi D siku  ya  Jumanne.

Hata  hivyo Argentina inalazimika  kuishinda  Nigeria  na  kuomba Iceland  isishinde dhidi  ya  Croatia, kwa  kuwa  hilo  linaweza kuwapeleka  Wamarekani  kusini hao nyumbani  na  mapema, ikitegemea tofauti  ya  magoli.

Brazil ilihitaji  jana mabao mawili  katika  dakika  za  majeruhi kuishinda  Costa Rica jana  wakati Philippe Coutinho  na  Neymar walipopachika  mabao na  kuwaweka  washindi  mara  tano  wa kombe  hilo katika  njia kuelekea timu 16 zitakazopambana  katika awamu  ya  mtoano.

Russland WM 2018 l Brasilien vs Costa Rica 1:0 Tor - Philippe Coutinho
Mshambuliaji wa Brazil Philippe Coutinho akishangiria bao la kwanza kwa timu yake dhidi ya Costa RicaPicha: Reuters/M. Rossi

Wabrazil  walionekana  kuelekea  katika  sare  yao  ya  pili  mfululizo yenye  kufadhaisha kabla  ya  mshambuliaji  wa Barcelona Coutinho kuuweka  mpira  wavuni kwa kupitia katikati  ya  miguu  ya  mlinda mlango  wa  Costa  Rica Keylor Navas  katika  dakika  ya 91  mjini St. Petersberg.

Neymar anyimwa penalti

Neymar, ambaye alikataliwa kupewa  mkwaju wa  penalti  na mwamuzi Bjorn Kuipers baada  ya  kuwasiliana  na wasaidizi  wa mwamuzi wanaohusika na  kuangalia vidio za  mchezo  huo , alifunga bao  la  pili  dakika  saba  katika  dakika  za  nyongeza. Lilikuwa bao la  hivi  karibuni  kabisa  katika  historia ya  kombe  la  dunia.

Russland WM 2018 l Brasilien vs Costa Rica - Neymar
Neymar anajiangusha lakini haitoshi kumzawadia mkwaju wa penalti dhidi ya Costa RicaPicha: Reuters/M. Brindicci

Ari  ya  Uswisi ya  kutokubali  kushindwa  na nia  ya  kutaka kushinda  ilikuwa funguo ya  kubadilisha  matokeo  katika  mchezo ambao  walisumbuliwa  na  Serbia  kwa  kipindi  kirefu cha  kwanza, kocha  wa  Uswisi Vladimir Petkovic  alisema  baada  ya  mchezo huo  ambao  Uswisi  ilishinda  kwa  mabao 2-1.

Mchezo  ulikuwa  katika  kasi  kubwa , ambapo Serbia  ilidhibiti mchezo katika  kipindi  cha  kwanza , lakini  Uswisi  ilianza  kwa  kasi kipindi  cha  pili na  kuiweka  Serbia  katika  wakati  mgumu.

Russland WM 2018 l Serbien vs Schweiz – 1:2 Tor
Xherdan Shaqiri (23)wa Uswisi anafunga bao la pili na la ushindi kwa Uswisi dhidi ya SerbiaPicha: Getty Images/C. Rose

Ujerumani  inarejea  dimbani  tena  leo ikipambana  na  Sweden katika  pambano ambalo Wajerumani  wanawania  kurejesha matumaini  yao  ya  kuendelea  mbele  katika  fainali  hizi baada  ya kipigo  cha  bao 1-0 dhidi  ya  Mexico  katika  mchezo  wao  wa ufunguzi  katika  kundi  F.

Russland WM 2018 | Deutschlands Training
Wachezaji wa timu ya Ujerumani wakifanya mazowezi wakisubiri pambano lao muhimu dhidi ya Sweden Picha: Getty Images/AFP/N. Almeida

Ujerumani  haitakuwa  katika  nafasi  nzuri  iwapo itatoka  sare na Sweden  ambayo  iliishinda  Korea kusini  katika  mchezo wa kwanza. Korea  kusini  pia  itakuwa  na  kibarua  kigumu  kuigaragaza Mexico  ambayo  nayo  pia  ina  pointi 3 baada  ya  kuilaza Ujerumani kwa  bao 1-0 katika  mchezo wa  kwanza.

Mchezo  wa  kwanza  hata  hivyo  leo ni  kati  ya Ubelgiji  na  Tunisia, ambayo  ilifanya  kazi  kubwa  katika  mchezo wake  wa  kwanza dhidi ya  Uingereza lakini  ikakubali  kipigo  cha  mabao 2-1 katika kundi  E.

Russland WM 2018- Fans von Marokko
Shabiki wa Tunisia akibeba kombe la mfano la dunia katika fainali zinazoendelea nchini UrusiPicha: Getty Images/AFP/F. Senna

Tunisia  inataka  kuendelea  kubakia  katika mashindano haya lakini  ina  mlima  mkubwa  wa  kupanda  kabl  ya  kutimiza ndoto  yao  hiyo hii leo  dhidi  ya  Ubelgiji  ambayo  iliirarua Panama kwa  mabao 3-0 katika  mchezo  wa  kwanza.

Mwandishi: Sekione Kitojo

Mhariri: Mohammed Khelef