1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Niger mwaka 2006 ilitumia tani nne za kuni

Siraj Kalyango11 Desemba 2007

Huko nako ni kuhatarisha kubadilka kwa hali ya hewa-kwani jangwa lanyemelea

https://p.dw.com/p/CaK7
Ramani ya Niger.Kusini mwake ni Nigeria-kaskazini ni Algeria ambazo zote zina utajiri wa mafuta na gesiPicha: DW

Misitu ya Niger –magharibi mwa Afrika-inazidi kutoweka.Mbali na maumbile kuchangia lakini pia binadamu nao wamechangia kwa sehemu sehemu moja kufikia hali hiyo.

Mapema alfajiri ukiwa mjini Niamey-mji mkuu wa Niger,utashuhudia mlolongo sio tu wa malori, lakini pia wa ngamia na punda,ukifululiza kuingia mjini.Shehena ya vyombo hivyo vyote vya usafiri ni mbao. Na mbao hizo hutolewa katika msitu pekee uliosalia nchini humo unaopatikana na katika sehemu za kusini –magharibi za nchi hiyo.

Kwa upande mwingine raia wa kawaida wanaendelea kukata ovyo miti katika misitu michache iliobaki kwa matumizi yao ya kawaida. Watu hao hawajali wala kuwa na habari za athari za vitendo vyao kuhusu kuongezeka kwa ujoto duniani ama kusambaa kwa jangwa ambalo linanyemelea karibu.

Wavuti moja ya kimazingira-Mongabay-unagusia hali inayoonyesha kuwa jangwa la Sahara, tayari limesha meza theluthi-mbili ya ardhi ya Niger na inaendelea kwa kasi ya hekta laki mbili kwa mwaka.

Jagwa linazidi kuijongelea nchi hiyo, licha ya mpango wake ilioutekeleza kati ya miaka 1985 na 1997.Mpango huo ulikuwa wa kupanda miti zaidi ya millioni 60.

Wataalamu wanasema kuwa jangwa linasambaa katika nchi hiyo kutoka sehemu za mashariki na kusini mwa nchi hiyo kuliko msitu pekee wa nchi hiyo.Wanaendelea kuwa kasi ya jangwa ni kilomita sita kila mwaka.Wavuti wa Mongabay unaendelea kusema kuwa kati ya miaka ya 1990 na 2005, Niger ilipoteza hekta, zaidi ya laki sita, za misitu, hii ikiwa zaidi ya theluthi-moja ya eneo lake zima lenye miti.

Wizara ya mazingira kwa upande wake, ingawa haitoi takwimu bayana, inakadiria kuwa hekta zisizopungua laki moja hupotea kila mwaka, ikiongezea zile hekta laki tatu zilizopotea kati ya mwaka wa 200 na 2006 katika mioto iliounguza misitu nchini humo.

Moja wa wachanja kuni na kuziuza katika soko la Dar-es-salaam, moja wa soko la mjini Niamey-Niger, asema kuwa ukataji miti umepungua.Hii ni kutokana na uhaba wa miti. Ameongeza kuwa wanabidi kutembea umbali wa kilomita zisizopungua 150 kuipta.

Mwaka wa 2006 nchi hiyo ilitumia karibu tani nne za kuni.Wadadisi wa serikali wanasema ifikapo mwaka wa 2010, inakisiwa karibu tani nne unusu za kuni ndio zitakuwa zikitumiwa kila mwaka.

Afisa mmoja wa shirika lisilo la kiserikali nchini humo, ameliambia shirika la habari la kifaransa la AFP kuwa Niger licha ya kuwa na utajiri wa makaa ya mawe na kuzungukwa na nchi zilizo na mafuta pamoja na gesi, matumizi ya kuni kama nishati majumbani yanafikia asilimia 90.Niger inapakana na Nigeria upande wa kusini ilhali Algeria iko upande wa kaskazini.

Hata hivyo mtaalamu moja ambae hakutaka jina lake litajwe alitambua kuwa umaskani katika nchi hiyo nao unachangia. Watu huishi kwa kutumia dola moja kwa siku katika nchi mojawapo wa maskini duniani, hawawezi kumudu bei ya mafuta na tena wakati huu ambapo bei ya mafuta na gesi imepanda.

Lakini yeye afisa kutoka shirika la Niger la maji na misitu- Mamane Lamine, amesema kuwa umaskini na kutojua si visingizio tosha kutenda alichikiita uhalifu wa kimazingira.

La kushangaza mjini Niamey mbao ni bidhaa ghali inaweza kufananishwa na dhahabu.Lori moja la mbao linauzwa kati ya dola 400 na 700.Na shehena ya ngamia moja ama punda zaidi ya Dola nne.

Shehena ya mbao au miti hutumiwa kwa kupikia mjini Niamey.Wakuu wa baraza la mji huo,ambao hutoza ushuru kwa mauzo ya miti hiyo,wanakiri kuwa hawana uwezo wa sekta amabyo inaongozwa na wafanya biashara wakubwa.

Na kwa wajumbe wa mkutano wa hali ya hewa wa Bali –Indonesia, kutoweka kwa misitu kuna athari tatu.Jua huichoma ardhi moja kwa moja bila kinga yoyote, hakuna kinga yoyote kuzuia upepo na hewa yenyewe huwa kavu.Na kwa upande mwingine kuenea kwa jangwa, kukisaidiwa na ukosefu wa mvua, ni moja wa sababu za uhaba wa chakula ulioikumba Niger ambayo idadi yake ya watu inaongezeka kwa asili mia tatu zaidi kwa mwaka.

Kwa mara nyingine bila kutoa takwimu taslimu, serikali inakadiria kuwa mwaka wa 1975, Niger ilikuwa na miti mingi mara 30 zaidi na ilio nayo kwa sasa.