Niebel azuru Kenya
15 Agosti 2012Ziara hiyo ina lengo la kuadhimisha miaka 50 ya ushirikiano wa pamoja kati ya makanisa mawili yenye miradi yake nchini Kenya. Pamoja na kukagua miradi kadha pia kutakuwa na mazungumzo ya kisiasa , hususan na waziri mkuu Raila Odinga.
Orodha ya mataifa washirika katika ushirikiano wa maendeleo ni ndefu, na ina idadi karibu ya majina 60. Kenya ni moja kati ya washirika muhimu wa ushirikiano huo, ambapo waziri Dirk Niebel anaizungumzia kama " nguzo ya uthabiti", katika Afrika mashariki.
Tathmini hii ya waziri Niebel kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na ushirikiano , ina misingi tofauti ya kimsingi. Na si kitu cha kushangaza basi , kwamba mwanasiasa huyu wa Ujerumani katika muda wa mwaka mmoja, hii inakuwa mara yake ya tatu kwenda Kenya.
Mwezi August mwaka 2011 Niebel alikutana na rais wa Kenya Mwai Kibaki na kutembelea kambi ya wakimbizi ya Daabab , kambi ambayo inawahifadhi watu kutoka katika nchi ya Somalia inayokabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mwanzoni mwa maafa ya ukame katika eneo la Afrika mashariki, ambapo hata Kenya iliathirika , kambi hiyo ambayo ilikuwa tayari na wakimbizi wanaofikia nusu milioni ilivuka kiwango cha uwezo wake wa kuwahifadhi wakimbizi.
Ujerumani inajihusisha tayari kwa miaka mingi pamoja na miradi inayoendeshwa na umoja wa mataifa katika kambi hiyo ya Daadab. Kutokana na ukame na matokeo yake waziri wa maendeleo ya Ujerumani Niebel aliongeza misaada kwa mataifa ya eneo hilo lote.
Pekee Kenya ilipata kiasi cha euro milioni 50 kwa mujibu wa taarifa rasmi za serikali.
Mwanzoni mwa mwezi Februari mwaka huu waziri Niebel alifanya ziara katika eneo la Turkana lililopo katika mpaka na Sudan ya kusini na kueleza kuwa hali katika eneo hilo ni ya dharura. Miezi sita imepita tangu wakati huo. Na kwa kuwa mwanasiasa huyo wa Ujerumani atatumia siku tano katika ziara yake nchini Kenya , ni dhahiri kuwa suala la ukame litakuwa mada muhimu ya mazungumzo.
Mbali na msaada wa kibinadamu , Niebel analenga kuchukua hatua endelevu ya kuisaidia Kenya.
"Katika ziara hii mbali na mazungumzo ya kisiasa tutatembelea pia miradi inayoendeshwa na makanisa ya Kiinjili na Kikatoliki. Tunaweza kufungua mradi wa pande tatu pamoja na Israel katika ziwa Viktoria.
Waziri mkuu wa Kenya atakuwapo na mwakilishi wa waziri wa mambo ya kigeni wa Israel. Hii inaonyesha , ni muhimu kiasi gani ushirikiano huu kwa serikali hizi tatu. Na ningependa kutumia fursa hii, kuitembelea taasisi ya umoja wa mataifa ya mazingira UNEP. Baada ya mkutano wa mazingira mjini Rio hiyo ni mada muhimu sana".
Katika mradi kati ya Ujerumani , Israel na Kenya ,mradi huo unahusu ufugaji wa samaki ulioanzishwa mwaka 1984. Mradi huo unahusu ufugaji wa aina ya samaki wa Sato, "Tilapia", ufugaji wa kuku, ng'ombe wa maziwa, mbegu za mimea ya matunda na miti.
Katika maendeleo ya kisiasa Kenya itaendelea kupata usaidizi kutoka Ujerumani. Mwishoni mwa mwaka 2010 nchi hiyo baada ya majadiliano na serikali , ilipata ahadi ya kupatiwa euro milioni 130 kwa muda wa miaka mitatu. Mazungumzo mengine yatafanyika katika muda wa miaka miwili ijayo katikati ya mwaka 2013, baada ya uchaguzi nchini Kenya.
Mwandishi : Fürstenau, Marcel / ZR/ Sekione Kitojo.
Mhariri: Othman Miraji