1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni siku ya maamuzi Kenya

4 Machi 2013

Zoezi la upigaji kura nchini Kenya lililoanza saa 12 alfajiri leo 4.3.2013 bado inaendelea huku milolongo mirefu ya wapiga kura ikiendelea kushuhudiwa katika vituo mbali mbali. Lakini mauaji huko pwani yamelitia doa.

https://p.dw.com/p/17poR
Wapiga kura wakiwa katika foreni wakisubiri kuchagua wawakilishi wao.
Wapiga kura wakiwa katika foreni wakisubiri kuchagua wawakilishi wao.Picha: Reuters

Wagombea urais wakuu Uhuru Kenyatta na Raila Odinga tayari wamepiga kura zao huko Gatundu na Kibera mtawalia. Mwandishi wa DW mjini Nairobi Alfred Kiti anasema milolongo mirefu ya wapiga kura bado inashuhudiwa katika vituo mbali mbali jijini humo, na kwamba wengi wa wapiga kura waliwasili vituoni kuanzia saa saba za usiku.

Hali ilivyokuwa katika mji wa Kisumu mapema leo.
Hali ilivyokuwa katika mji wa Kisumu mapema leo.Picha: Reuters

Mjini Nairobi hakukua na visa vyovyote vya mtafaruku vilivyoshughuliwa ingawaje baadhi ya vituo vimeripotiwa kuwa na hitilafu ya mitambo ya kutambua wapiga kura jambo ambalo limechelewesha shughuli hiyo katika vituo kadhaa. Tatizo hili limeripotiwa pia mjini Kisumu nam Mwandishi wa DW alieko huko John Marwa.

Wagombea wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda ni Waziri Mkuu Raila Odinga na Naibu wake Uhuru Kenyatta. Odinga alipiga kura yake mapema huko Kibera, huku Kenyatta akipiga ya kwake katika eneo la Gatundu. Odinga amesema Wakenya wanayo nafasi ya kuamua kama kweli wanataka mabadiliko, huku Kenyatta akiahidi kuheshimu maamuzi ya Wakenya, inagawa ailionyesha matumaini ya muungano wake wa Jubili kushinda katika duru hii ya kwanza.

MRC yadaiwa kufanya mauaji Mombasa

Wakati huo huo Inspekta Mkuu wa Polisi Davisd Kimaiyo amesema maafisa 400 wa polisi wamepelekwa huko Mombasa ambako kumetokea makabiliano kati ya maafisa wa polisi na watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa kundi la Mombasa Republican Council - MRC.

Waziri Mkuu Raila Odinga akipiga kura yake katika eneo la Kibera.
Waziri Mkuu Raila Odinga akipiga kura yake katika eneo la Kibera.Picha: Reuters

Wafuasi wa kundi hilo wanadaiwa kufanya mashambulizi asubuhi ya leo, na kuua watu wasiyopungua 15 wakiwemo maafisa sita wa Polisi mjini Mombasa. Afisa mwinfine wa Polisi pia aliuawa katika shambulio mkoani Kilifi, kilomita 50 kaskazini mwa Mombasa.

Raila Odinga na Uhuru Kenyatta walilaani mashambulizi hayo na kuyayita ya kihaini. Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC Ahmed Issack Hassan naye alilaani mashambulizi hayo, ikiwa ni pamoja na yale yaliyotokea katika mji wa kaskazini-mashariki wa Garissa. Mkuu huyo wa IEBC pia alikiri kutokea kwa matatizo ya usafirishaji wa vifaa vya kupigia kura pamoja na wasimamizi.

Waangalizi nao wanena

Mkuu wa timu ya waangalizi kutoka Umoja wa Ulaya, Alojz Peterle alisema ripoti za awali zimeonyesha kuwa vituo vingi vya kupigia kura vilifunguliwa kwa wakati, na kumekuwepo na mwitikio mkubwa wa wapiga kura ambao wameonyesha uvumilivu na utulivu wa hali ya juu.

Maafisa watume ya uchaguzi wakihakiki majina ya wapiga kura katika kituo cha Shule ya Kileleshwa mjini Nairobi.
Maafisa watume ya uchaguzi wakihakiki majina ya wapiga kura katika kituo cha Shule ya Kileleshwa mjini Nairobi.Picha: DW

Waangalizi wa uchaguzi huo kutoka jumuia ya Commmonwelath, Umoja wa Ulaya , Umoja wa Afrika Jumuia ya Afrika Mashariki, The Carter Centre na Shirika la IGAD na COMESA wametoa taarifa ya pamoja kuwataka wanasiasa na vyama vyao kuzingatia kanuni za tume huru ya uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani.

Kulingana na idadi ya watu waliojitokeza kwenye shughuli ya leo huenda wengi wakakosa nafasi ya kupiga kura kwani vituo vinatakiwa kufungwa saa kumi na moja jioni kulingana na kanuni za Tume ya uchaguzi IEBC.

Mwandishi: Alfred Kiti/ Iddi Ssesanga/AFPE
Mhariri: Josephat Charo