1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni kosa kupanga tarehe ya kuondoka Afghanistan

19 Machi 2010

<p>Mshauri wa masuala ya usalama wa Rais Karzai wa Afghanistan ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutopanga tarehe ya kuondoka Afghanistan. Amesema, kufanya hivyo ni kutuma risala potofu kwa umma na magaidi.

https://p.dw.com/p/MWco
Afghanistan's Froeign Minister Rangin Dadfar Spanta looks on during the EU Troika-Afghanistan plenary meeting of Ministers at the Cernin's Palace in Prague, Czech Republic, Wednesday, Jan. 28, 2009. (AP Photo/Petr David Josek)
Rangin Dadfar Spanta,mshauri wa masuala ya usalama katika serikali ya Rais Hamid Karzai wa Afghanistan.Picha: AP

Picha inayotolewa na mshauri wa masuala ya usalama, Rangin Dadfar Spanta, inatisha. Anasema: ikiwa nchi za Magharibi zitaondoka Afghanistan mapema mno, basi magaidi wa kitaifa watakuwa na mahala pa kujificha kwa usalama na kueleza hivi

"Hiyo itamaanisha kupoteza yote yaliyopatikana: kuanzia elimu,uhuru wa vyombo vya habari, huduma za afya na haki za binadamu."

Spanta alieishi Ujerumani muda mrefu, alihusika na harakati za kisiasa, na siku hizi hufuatiliza midahalo inayoendelea Ujerumani na inamtia wasiwasi. Kwa hivyo, anaonya dhidi ya mambo mawili : kuondoka mapema na hata kupanga tarehe maalum ya kuondoka Afghanistan.Amesema:

"Hiyo itatuma ujumbe potofu pande mbili: Kwanza ni kwa umma wa Afghanistan kuwa tunaondoka bila ya kuwaachieni mazingira yanayohitajika:  Na kwa magaidi, ni kama kuwaambia kuwa baada ya mwaka au miaka miwili mtaweza kufanya mtakalo kwani vyo vyote vile, sisi tunaondoka."

Anasema anaelewa wasi wasi wa umma wa nchi zinazopeleka majeshi yake Afghanistan, hasa Ujerumani ambako wananchi wengi, wanapinga wanajeshi wao kuwepo Afghanistan.  Wakati huo huo, anaonya kuwa Wajerumani wasipuuze kitisho cha magaidi, kwani walioshambulia miji ya Madrid na London walifunzwa na walitumwa Ulaya na wale wanaopigwa vita hivi sasa nchini Afghanistan.

Mtu asiamini kuwa anaweza kujitenga na kuendelea maisha yake ya neema barani Ulaya bila ya kudhuriwa na magaidi. Spanta amesisitiza kuwa adui mkubwa kabisa wa Taliban si mkulima wa Afghanistan, bali demokrasia, haki za wanawake, haki za binadamu na mtindo wa maisha katika nchi za Magharibi.

Kwa maoni yake, mwaka huu machafuko yataongezeka nchini Afghanistan. Yeye anaamini kuwa vurugu litazidi kabla ya hali ya utulivu kupatikana. Migogoro yote ya kijeshi anasema, humalizika kwa majadiliano ya amani. Kwa hivyo, kila hatua ichukuliwe kuwasaidia walio tayari  kufungua ukurasa mpya na kuishi kwa amani, isipokuwa wale wanaokataa kujitenga na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda. Lakini mshauri huyo wa masuala ya usalama katika serikali ya Karzai amesisitiza na tunamnukuu " Tukilazimika kupigana basi tutapigana." mwisho wa kumnukuu.

Mwandishi:Küstner,Kai/ZPR/P.Martin 

Mhariri: Othman,Miraji