Ngoma bado nzito Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.06.2012
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ngoma bado nzito Syria

Mapigano makali yalioanza Jumanne jioni na kuendelea usiku kucha katika mkoa wa Latakia, kaskazini magharibi mwa Syria yamesababisha vifo vya watu 39, wakiwemo wanajeshi wa serikali wasiopungua 20.

Moshi ukifuka mkoani Homs kufuatia mashambulizi.

Moshi ukifuka mkoani Homs kufuatia mashambulizi.

Mapigano hayo yalianza saa chache baada ya kiongozi wa timu ya waangalizi wa amani wa Umoja wa Mataifa kuliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa timu yake itaendelea kuwepo nchini Syria hadi pale suluhisho la kisiasa litakapopatikana.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Ufaransa AFP, wanajeshi 28 wa serikali na waasi watano waliuawa katika mapigano hayo yaliyotokea katika mkoa ambao unafahamika kama Mlima wa Wakurdi karibu na mpaka wa Uturuki.

Kiongozi wa Shirika la uangalizi wa haki za binadamu nchini Syria, Rami Abdul Rahman, alisema wengi wa wanajeshi hao waliuawa katika makabiliano ya moja kwa moja na waasi, wakati wengine waliuawa katika uvamizi kwenye majengo mawili yaliyokuwa yanatumika na jeshi kufanya mashambulizi ya roketi dhidi ya mlima wa Wakurdi.

Mwanajeshi wa Jeshi Huru la Syria akifytua risasi wakati wa mapambani na wanajeshi wa serikali.

Mwanajeshi wa Jeshi Huru la Syria akifytua risasi wakati wa mapambani na wanajeshi wa serikali.

Abdul Rahman alisema wanajeshi kadhaa akiwemo Afisa wa cheo cha juu pia walitekwa na waasi waliochukua pia silaha zao. Katika Idlib, mkoa mwingine uliopo kaskazini Magharibi karibu na mpaka wa Uturuki, wanajeshi watano wa serikali waliuawa wakati bomu lililotegewa ndani ya gari liliporipuka katika kizuizi usiku. Miripuko mingine na milio ya risasi ilisikika pia katika miji ya Maaret al-Numan.

Homs yazidi kulengwa
Na katika mkoa wa kati wa Homs, mapambano katika mji wa Kernaz yalisababisha vifo vya wanajeshi watatu, huku mashambulizi kutoka kwa vikosi vya serikali yakiuwa mwanamme moja na mke wake. Kiongozi wa Kishia, Sayyida Zeinab aliuawa na watu wenye silaha ambao hawakuweza kutambulika kusini mwa Damascus, palipo na eneo takatifu wa waumini wa shia na ambako kulitokea mripuko wa kujitoa mhanga Juni 14.

Shirika hilo lilisema wanajeshi wa serikali walimuua kwa risasi raia moja katika kizuizi katika eneo la Harasata, kaskazini mashariki, wakati afisa wa jeshi la waasi alikufa kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa mapambano hapo awali.

Wakati huo huo, shirika la habari la Ujerumani, DPA, limeripoti kuwa majeshi ya serikali yameendelea na mashambulizi dhidi ya ngome za wapinzani leo na kuua watu wasiopungua watano. Katika mkoa wa Homs, vikosi hivyo viliyalenga maeneo ya Khalidiya, Jouret al-Jouz na Kussair, ambapo watu watatu waliuawa.

Rais wa Marekani Barack Obama alikutana na Rais Vladmir Putin wa Urusi kando mwa mkutano wa kilele wa mataifa ya G20 huko Mexico, na kujadili miongoni mwa mambo mengine, hali nchini Syria ambapo wote walielezea matumaini yao ya kuona mgogoro huu unafikia mwisho.

Kiongozi wa timu ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa, Meja Jenerali Robert Mood.

Kiongozi wa timu ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa, Meja Jenerali Robert Mood.

"Tumejadili masuala ya usalama. Tumezungumzia ushirikiano wa kiuchumi, kwa maoni yangu naona tuna mambo mengi yanayotukutanisha na matatizo mengi ya kimataifa, likwemo suala la Syria. Tutaendelea kuyazungmzia katika ngazi zote, alisema Putin baada ya mkutano huo. Marekani imekuwa ikiishtumu Urusi kwa kuendelea kuipa Syria silaha, jambo ambalo Urusi inakanusha.

Kampuni ya Urusi yakanusha kupeleka silaha Syria
Wakati huo huo kampuni ya Urusi ya kusafirisha mizigo imekanusha kupeleka silaha na zana nyingine za kivita nchini Syria. Kampuni hiyo ya Femco ilidaiwa kusafirisha helikopta za kivita kwa kutumia meli yake ya MV Alaed, kwa mujibu wa gazeti la Uingereza la Sunday Telegraph.

Lakini Kampuni hiyo ilisema katika taarifa yake kuwa meli hiyo ilipeleka helikopta za kivita aina ya Mi-25 kutoka bandari ya Kiliningrad zilikokuwa zimepelekwa kwa ajili ya matengenezo. Femco ilisema meli yake inasafirisha mizigo kufuatana na masharti ya kimataifa, na kwamba wateja wake wanaiamini kuwa ni kampuni safi.

Kampuni ya bima ya Insurer Satndard Club ilisema mwanzoni mwa wiki kuwa ilikuwa imesimamisha huduma za bima kwa meli hiyo ya MV Alaed, jambo ambalo linaifanya meli hiyo isiweze kufanya zake hadi pale mmiliki atakapopata bima nyingine.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE\DPAE
Mhariri: Mohammed Khelef

 • Tarehe 20.06.2012
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Maneno muhimu Syria, mambo bado
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/15IIJ
 • Tarehe 20.06.2012
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Maneno muhimu Syria, mambo bado
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/15IIJ

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com