1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Neymar akaribia kujiunga na PSG

Bruce Amani
2 Agosti 2017

Mshambuliaji nyota wa Barcelona Neymar amepewa ruhusa ya kuondoka klabu hiyo akitarajiwa kujiunga na Paris Saint Germain katika uhamisho unaokisiwa kugharimu kitita cha rekodi ya pauni milioni 198.

https://p.dw.com/p/2haS4
Spanien Fußball La Liga FC Barcelona - RC Celta de Vigo
Picha: Getty Images/A. Caparros

Alipewa ruhusa na kocha Ernesto Valverde asifanye mazoezi ya kabla ya msimu mpya na badala yake kushughulikia mpango wa uhamisho wake.

Mshambuliaji huyo ataruhusiwa kuondoka kwa gharama ya Euro milioni 222, ambazo PSG iko tayari kulipa. Hayo yanajiri siku mbili baada ya kubainika kwamba Barca ilikuwa tayari kuruhusu uchunguzi wa Fifa iwapo PSG ingemsajili Neymar.

Katika mahojiano na gazeti la Mundo Deportivo, rais wa La Liga Javier Tebas alitishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mabingwa hao wa zamani wa Ligue 1 iwapo soka ya Ulaya itashindwa kuchukua hatua.

Aidha alisema kuwa Rais wa PSG Nasser Al Khelafi alijulishwa kuhusu malengo ya miamba hao wa Uhispania.

Neymar alihamia Barcelona kutoka klabu ya Santos ya Brazil mwaka wa 2013 kwa uhamisho wa pauni £46.6m na kusaini mkataba wa miaka mitano na mabingwa hao wa Uhispania 2016.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Iddi Sessanga